Jammeh aahidi mwisho wa amani kwa mgogoro Gambia
11 Januari 2017Katibu mkuu wa chama tawala ndiye atafanya upatanishi kati ya wafuasi wa Jammeh na upande wa upinzani ili kutatua hali yoyote ya kutokuaminiana na masuala mengine, alisema Jammeh katika hotuba kwa taifa iliotangazwa moja kwa moja kwa njia ya televisheni mapema siku ya Jumatano.
Jammeh anakataa kukubali matokeo ya uchaguzi kwa sababu anadai yalikuwa na makosa mengi ya kimahesabu na kasoro kadhaa, na hayakuweza kutolewa ufafanuzi unaoaminika, aliongeza kusema rais huyo anaemaliza muda wake.
Jammeh amemuamuru waziri wa sheria na bunge kuandaa muswada wa sheria ya msamaha, huku akitoa agizo la rais pia la kutowakamata au kuwashtaki raia kwa vitendo au makosa yaliotendwa wakati wa kipindi cha kuelekea na baada ya uchaguzi, kati ya Novemba Mosi na Januari 31.
Tangazo hilo lilikuja siku moja baada ya mahakama ya juu kabisa kuahirisha usikilizaji wa kesi iliyowasilishwa na Jammeh kupinga matokeo ya uchaguzi. Kesi iliahirishwa hadi siku ya Jumatatu, kwa sababu mmoja tu kati ya majaji watano wanaohitajika ndiye alikuwepo, karani wa mahakama hiyo aliliambia shirika la habari la Ujerumani DPA.
Matumaini kiduchu ya kusikilizwa kesi
Wataalamu wanaamini hata hivyo, kwamba itakuwa vigumu sana kwa majaji wanne kuwepo siku ya Jumatatu, kwa sababu mahakama ya juu imekuwa haifanyi kazi tangu Jammeh alipowafuta kazi majaji kadhaa wa mahakama hiyo katikati mwa mwaka 2016.
Majaji wengine wote wenye vigezo kutoka mahakama ya rufaa waliitoroka nchi hiyo baada ya uchaguzi wa Desemba. Barrow, ambaye ni mfanyabiashara wa zamani wa uuzaji majumba ambaye hakuwa anajulikana sana kabla ya kutangaza nia ya kuwania kiti cha urais, alisema katika taarifa kwamba anapanga kuingia ofisini Januari 19 kama ilivyopangwa.
"Haki ya mshindi kuapishwa kuwa rais na wajibu wa rais wa sasa kuondoka madarakani pale muda wake unapomalizika havibatilishwi na kuwasilisha pingamizi la uchaguzi," alisema rais huyo mteule mwenye umri wa miaka 51.
ECOWAS yajiandaa kutuma jeshi
Viongozi kadhaa wa mataifa ya Afrika Magharibi wameahirisha mkutano na Jammeh uliolenga kusaidia kutatua mgogoro huo wa kisiasa kutoka siku ya Jumatano hadi Ijumaa. Nigeria ilisema ucheleweshwaji huo ulitokana na Jammeh kushikilia iwe hivyo. Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zinatarajiwa kushiriki mazungumzo hayo na kumtolea wito Jammeh kuheshimu katiba ya nchi yake.
Jumiya ya ECOWAS imesema imeliweka tayari jeshi lake ikiwa Jammeh atakataa kukabidhi madaraka wakati muhula wake utakapomalizika Januari 19. Jammeh alitwaa madaraka katika mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu mnamo mwaka 1994, lakini anatuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliohusisha ufungwaji wa wapinzani wake kiholela, mateso na mauji ya wapinzani katika taifa hilo dogo la watu milioni 1.9.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/Dpae
Mhariri: Grace Patricia Kabogo