Jammeh aapa kutoondoka madarakani
23 Desemba 2016Msimamo wa Jammeh umezusha wasiwasi kimataifa juu ya hali ya baadaye ya taifa hilo dogo la Afrika magharibi, wakati Umoja wa Afrika ukijiunga na viongozi wa Afrika kumtaka ajiuzulu.
Jammeh alisema katika hotuba ndefu katika televisheni, kwamba haki zake haziwezi kukiukwa na kukandamizwa na hatasalimu amri ya ECOWAS.
Gambia inakabiliwa na mkwamo wa muda mrefu wa kisiasa baada ya kiongozi huyo wa muda mrefu kusema atasubiri hadi uamuzi wa mahakama utakapopatikana Januari kabla ya kukabidhi madaraka.
Jammeh, ambaye amekuwa madarakani kwa muda wa miaka 22, aliwashangaza wadadisi kwa awali kukubali kushindwa katika uchaguzi wa Desemba Mosi dhidi ya mpinzani wake Adama Barrow, lakini kubadilika wiki moja baadaye, akikataa matokeo na kuwasilisha pingamizi mahakamani.