Jammeh akataa kuondoka madarakani
21 Desemba 2016Jammeh alishindwa katika uchaguzi wa Disemba Mosi na mgombea wa mwanasiasa asiyefahamika sana na aliyeungwa mkono na muungano wa upinzani, Adama Barrow, na kwa mshangao wa wengi akakubali haraka kushindwa huko lakini wiki moja baadaye akabadilisha kauli yake, akidai uchaguzi ulikuwa na kasoro kubwa.
Kwa upande wake, Barrow amejaribu kupunguza hali ya wasiwasi kwa kuahidi kwamba Jammeh hatakabiliwa na mashitaka ya aina yoyote akiondoka madarakani. Mara tu baada ya mgombea wao kutangazwa kuwa mshindi, baadhi ya maafisa wa upinzani walikuwa wametoa kauli zinazoashiria kuwa Rais Jammeh angelikabiliwa na mashitaka kwa ukatili na mauwaji dhidi ya wapinzani wake.
Jammeh anashutumiwa na makundi ya haki za binadamu kwa kuwaweka kizuwizini kuwatesa na kuwauwa wale wanaoshukiwa kuwa wapinzani katika muda wa uongozi wake wa miaka 22.