Jaribio la mapinduzi Uturuki; hali yadhibitiwa
16 Julai 2016Uturuki iliingia katika mtafaruku mapema usiku wa manane kuamkia leo Jumamosi , wakati hali ya mapinduzi ya kijeshi ilipokuwa inajitokeza, wakati hakuna uhakika jaribio hilo la mapinduzi limesambaa kwa kiasi gani, ama ni nafasi gani jaribio hilo linaweza kufanikiwa.
Kundi ndani ya jeshi la ulinzi la nchi hiyo limefanya jaribio la kuipindua seriaki iliyochaguliwa kidemokrasia, amesema afisa katika ofisi ya rais Recep Tayyip Erdogan, ambae inaonekana hajaondolewa katika wadhifa wake.
Afisa huyo amesema taarifa ya hapo kabla ya jeshi la Uturuki ikitangaza kuchukuliwa madaraka na jeshi haikutolewa na uongozi wa juu wa jeshi, ikiashiria kwamba mapinduzi hayo huenda yamefanywa na kundi la wanajeshi waliojitenga.
Tovuti ya jeshi la Uturuki ilikuwa haipatikani , ikiwa inazidi kuzusha maswali juu ya wale ambao wanahusika na jaribio hilo la mapinduzi.
Wahusika wa jaribio hilo
Taarifa ya awali ya kutangaza mapinduzi ilisomwa na mtangazaji aliyekuwako studio ya televisheni ya TRT. Pia alitangaza kwamba kulikuwa na amri ya kutotoka nje nchini humo hadi itakapotangazwa vinginevyo, ikielezea haja ya watu kuwa na usalama.
kulikuwa na taarifa za ndege za kivita kuruka chini chini katika anga ya Istanbul, pamoja na milio ya risasi na miripuko katika mji huo.
Baadaye rais Erdogan alipiga simu katika kituo cha televisheni cha CCN Uturuki na kusema yuko salama, na kuwataka watu kujitokeza kupinga mapinduzi hayo.
Japokuwa wakati huo ulikuwa usiku mkuu wa manane lakini maelfu ya watu walijitokeza barabarani kuunga mkono wito wa Erdogan na walimiminika mjini Istanbul kwa wingi.
Kiongozi wa jaribio la mapinduzi
Hapo mapema waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim alisema katika televisheni moja nchini humo kwamba kumekuwa na jaribio la mapinduzi, lililofanywa na baadhi ya wanajeshi.Ameahidi kwamba demokrasia haitapinduliwa.
Taarifa zinasema afisa ambaye ameondolewa katika nafasi yake hivi karibuni kama mshauri wa masuala ya sheria katika jeshi la Uturuki, aliyetambuliwa kama Muharrem Kose , ndie anayeongoza jaribio hilo linaloendelea na mapinduzi, linaripoti shirika la habari la Anadolu.
Kamanda wa kikosi cha kwanza cha jeshi la Uturuki , kikiwa ni sehemu ya jeshi la ardhini la Uturuki linalohusika na ulinzi mjini Istanbul pamoja na maeneo mengine ya upande wa magharibi nchini humo, amesema wale wanaofanya jaribio la mapinduzi ni kikundi kidogo na hakuna kama alivyosema cha kuhofia.
Majeshi yalifyatua risasi dhidi ya kundi la watu waliokusanyika mjini Istanbul kufuatia jaribio hilo la mapinduzi, na kusababisha maafa, amesema mpiga picha mmoja wa shirika la habari la AFP.
Shirika la habari la serikali Anadolu , limeripoti polisi 17 wameuwawa katika shambulio dhidi ya helikopta iliyokuwa na kikosi maalum cha polisi katika makao makuu ya polisi nje ya mji mkuu Ankara.
Televisheni nchini humo zimesema watu 42 wameuwawa, kwa mujibu wa mwendesha mashitaka nchini humo. Erdogan alitabiri kwamba mapinduzi hayo yatashindwa na waungaji mkono wa chama tawala cha AKP , Justice and Development Party walijitokeza mitaani kuzuwia mapinduzi hayo.
Wakati maafisa nchini Uturuki wakielezea kwamba mapinduzi yanadhoofika na Erdogan kuliamuru jeshi kuzitungua ndege zinazotumiwa na wale waliopanga njama za mapinduzi, waziri mkuu Binali Yildirim alisema watu 120 waliohusika katika mapinduzi wamekamatwa.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kupitia msemaji wake kwamba utaratibu wa kidemokrasia lazima uheshimiwe Uturuki.
Nae rais wa marekani Barack Obama amezitaka jana pande zote nchini Uturuki kuunga mkono serikali iliyochaguliwa kidemokrasia, baada ya jaribio hilo la mapinduzi.
Urusi imesema ina wasi wasi juu ya hali nchini Uturuki , baada ya majeshi ya nchi hiyo kuingia mitaani mjini Ankara na Istanbul na kutangaza mapinduzi.
Insert report.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Yusra Buwayhid