Je Libya, itashindwa kufanya uchaguzi wa Desemba?
28 Septemba 2021Wiki iliyopita baraza la wawakilishi, liliondoa uungaji mkono wake wa serikali ya umoja wa kitaifa ya mjini Tripoli. Tangu wakati huo waziri mkuu wa mpito wa Libya Abdul Hamid Mohammed Dbeibeh amebaki tu na jukumu la kuwa mwangalizi. Hata hivyo, hali hiyo mpya haipaswi kuathiri majukumu yake ya msingi ambayo yalikuwa ni kuandaa uchaguzi mkuu wa rais na bunge kulingana na mwongozo unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Hadi kufikia sasa, bunge limepitisha sheria pekee ya uchaguzi wa rais lakini sio wa bunge, ambao umepangwa kufanyika tarehe sawa na ile ya rais. Na hivi karibuni Dbeibeh alionyesha wasiwasi kwamba huenda nchi haiko tayari kwa uchaguzi.
Ni muhimu pia kuzingatia kwamba Dbeibeh mwenyewe hatowania urais. Ingawa, baadhi ya Walibya upande wa magharibi wasingepinga kugombea kwake. Sheria ya urais inasema wazi kwamba watumishi wa umma wanapaswa kujiondoa katika nafasi zao miezi mitatu kabla ya tarehe ya uchaguzi, kwa maana hiyo angepaswa kujiuzulu ili aweze kujiunga na kinyang'anyiro hicho.
Pengine hiyo ndio sababu ya kwa nini spika wa bunge Aguila Saleh alijiondoa katika nafasi yake mara tu baada ya kuidhinisha sheria ya uchaguzi wiki iliyopita. Virginie Collombier mtafiti wa mshikamano wa kisiasa wa Libya aliieleza DW kwamba "Aguila Saleh awali alikuwa kwenye orodha ya vikwazo, lakini aliondolewa na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa ili kuruhusu kipindi cha mpito kuendelea"
Collombier anashawishika kwamba jina jingine ambalo lilipaswa kuwamo katika orodha hiyo ya vikwazo ni la Jenerali Khalifa Haftar. Huyu ni mbabe wa kivita upande wa mashariki, na ambaye wiki hii aliachia wadhifa wake kama mkuu wa vikosi vya kiarabu vya Libya. Hii ni ishara kwamba huenda naye ana dhamira ya kuwania urais.
Mchambuzi mwingine Sami Hamdi kutoka kampuni inayojikita katika masuala ya maslahi ya kimataifa, vitisho vya kidunia na intelijensia ikiwa na makao yake mjini London, Uingereza, yeye pia anawatizama wagombea hawa wawili kutoka mashariki kwa mashaka. "Ukweli kwamba Haftar na Saleh wana dhamira ya kugombea, inaonyesha wazi kwamba hawazungumzi kwa sauti moja".
Kulingana na Hamdi, hata hivyo, Haftar yuko katika hali ya ushindi. "Kama atashinda atakuwa rais, kama atashindwa atarudi na kuongoza jeshi lake na kundelea kuwa na jeshi lenye nguvu upande wa mashariki".
Wagombea wengine wanatarajiwa kutangaza nia zao hivi karibuni. Saif al-Islam Gadafhi, mmoja wa watoto wa kiume wa hayati Moammar Gadafi ameashiria dhamira yake ya kuwania urais. Ushawishi wa Uturuki na Urusi nchini Libya ni mkubwa. Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba kuna zaidi ya wapiganaji 20,000 wa kigeni na mamluki kutoka Uturuki, Urusi, Sudan na Chad nchini Libya. Kwa umoja wa Mataifa kuondolewa kwao ni ajenda muhimu sana katika makubaliano ya kusitisha mapigano ya Oktoba mwaka uliopita na yaliyosafisha njia ya uchaguzi wa taifa.
Wachambuzi wanashawishika kwamba uchaguzi hautokuwa na athari kubwa kwa Walibya au jinsi wanavyochagua viongozi. Hamdi anasema unahusu "kuvileta vyama vya Libya na wababe wa kivita wa Libya kukubaliana na mwongozo wa kutawala au kushirikiana pamoja". Kwa mtizamo wake, uhalisia ungekuwa ni uchaguzi wa kitaifa ufanyike, walibya wapige kura na matokeo yakubaliwe na pande pinzani.
Hata hivyo, anahisi kwamba hapatakuwa na mshindi wa wazi na mahasimu wa kisiasa hawatakubaliana na matokeo ya uchaguzi, na hili litawarejesha katika hali ilivyokuwa awali ikiwemo serikali dhaifu, mgawanyiko baina ya mashariki na magharibi na masuala ya kukosekana usalama.