JERUSALEM:Vikosi vya Israel vyaingia Jenin
9 Januari 2004Matangazo
Vikosi vya Israel vimeingia katika mji wa Ukingo wa Magharibi wa Jenin mapema leo asubuhi na kuwakamata Wapalestina 15 pamoja na kushambuliana kwa risasi na wanamgambo. Leo pia Israel imesema itajaribu kuwapunguzia vikwazo Wapalestina ili kuepusha maafa ya kibinaadamu yanayozidi kuongezeka katika maeneo ya Wapalestina. Hatua hizo zinakuja siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Palestina Ahmed Qorei kuonya kwamba iwapo Israel itachukuwa hatua ya upande mmoja kusawiri mpaka mpya na maeneo ya Wapalestina atajibu kwa kuchukuwa hatua ya kushinikiza kuanzishwa kwa taifa moja la Kiarabu na Kiyahudi hatua ambayo itaashiria maafa kwa Israel. Nchi moja itakayojumuisha Gaza,Ukingo wa Magharibi na Israel itamaanisha kwamba taifa hilo la Kiyahudi litakuwa na wananchi wengi wa Kiarabu kuliko Wayahudi na kuilazimisha Israel kuchaguwa kati ya kuwapa Wapalestina haki ya kupiga kura na hiyo kupoteza umbile la Kiyahudi la taifa hilo au kuwa nchi ambapo walio wachache ndio wanaotawala kama ilivyokuwa Afrika Kusini wakati wa utawala wa kibaguzi. Waziri Mkuu wa Israel Ariel Sharon alionya mwishoni mwa mwaka jana kwamba ataamuru kujitenganisha na maeneo ya Wapalestina iwapo mazungumzo ya amani hayatoonyesha maendeleo katika miezi inayokuja. Waziri Mkuu wa Palestina Ahmed Qorei ameliambia shirika la habari la Associated Press hapo jana kwamba hatua hizo za upande mmoja zitazifanya harakati za kupigania taifa la Palestina kuwa kauli mbiu isiokuwa na maana na kwamba iwapo hali itaendelea kama ilivyo hivi sasa watapigania kuwa na taifa moja kama uvumbuzi wa mgogoro huo wa Mashariki ya Kati.
Matangazo