Jeshi la Sudan kushiriki mazungumzo ya Geneva
16 Agosti 2024Hatua hii inakuja baada ya shirika la habari la Sudan SUNA, kuripoti kuwa mtawala wa kijeshi wa Sudan Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alikubali kushiriki mazuingumzo hayo kwa sharti kwamba yanaoongozwa na wapatanishi wa mchakato wa amani wa Jeddah uliokwama Desemba iliyopita.
Shirika la SUNA limeripoti hapo jana kuwa Burhan, ambaye ni mwenyekiti wa Baraza Tawala la Sudan alifafanua kuwa hakuna kipingamizi kwa kukaa na wawezeshaji wa jukwaa la Jeddah kujadili nao namna ya kutekeleza Tamko la Jeddah na kukariri kwamba Sudan inapingaa kutanuliwa kwa idadi ya wapatanishi.
Mnamo Agosti 14, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alifany amazungumzo kwa njia ya simu na Burhan na kumhimiza kutuma ujumbe wa jeshi kwenye mazungumzo hayo.
Shirika binafsi la Tovuti binafsi ya El Balad News liliripoti jana likinukuu vyazo vya Sudan, kwamba ujumbe wa jeshi la Sudan unatarajiwa kuwa Geneva leo.
Jeshi lilikuwa limesusia mazungumzo ya Geneva na mahasimu wao kutoka kundi la wanamgambo wa RSF na wadau wengine wa Sudan, ambayo yalifunguliwa Agosti 14, baada ya kutoa masharti kadhaa ya kushiriki mazungumzo hayo, ikiwemo utekelezaji wa Tangazo la Jeddah na kuondolewa kwa Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE.
Soma pia:Marekani yalisisitizia jeshi la Sudan kuhudhuria mazungumzo ya amani
Hapo jana mjumbe wa Marekani anaeongoza majadiliano hayo Tom Perriello, aliarifu kuwa jeshi la Sudan lilikuwa bado linajitenga na mazungumzo, lakini akaongeza kwamba walikuwa wanaendelea kuwa na mawasiliano nalo kila siku, na kupiga hatua kuhusu msaada wa kibinadamu.
Alisema uongozi wa mazungumzo hayo ulikuwa unazungumza na pande zote mbili, wakitumia simu kuwasiliana na jeshi la Sudan, SAF, huku ujumbe wa RSF ukiwa nchini Uswisi.
"Ukweli ni kwamba, katika siku na zama hizi, kila mmoja katika muungano huu wa kidiplomasia naweza kuzungumza na uongozi wa Jeshi la Sudan na RSF kila siku," Alisema mjumbe huyo wa Marekani kwa Sudana.
"Huku tukijikita katika chumba juu ya nini tunaweza kufanya pamoja kujaribu kufungua mipaka zaidi na njia kwa ajili ya chakula na dawa, kupata siku zaidi kwa raia wanaokimbia mashambulizi."
Mazungumzo yaendeshwa kwa faragha
Mazungumzo hayo yanaendeshwa kwa pamoja kati ya Marekani, Saudi Arabia na Uswisi, huku Umoja wa Afrika, Umoja wa Falme za Kiarabu na Umoja wa Mataifa zikifanya kama kundi la kupanga vipaumbele.
Majadiliano hayo yalioanza siku ya Jumatatu na yanaweza kudumu kwa karibu siku 10, yanafanyika kwa faragha na katika eneo ambalo halijatajwa.
Vita vimerindima nchini Sudan tangu Aprili 2023 kati ya jeshi linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan na RSF iliyo chini ya aliekuwa naibu wake Mohamed Hamdan Daglo.
Soma pia:Marekani kuanzisha mazungumzo ya amani ya Sudan, licha ya jeshi kutothibitisha
Vita hivyo vimesababisha mmoja ya mizozo mibaya zaidi ya kiutu duniani. Raia wa Sudan hata hivyo wanaonyesha mitazamo tofauti kuhusu mazungumzo hayo, kama anavyosema mkaazi huyu wa Port Sudan, Mousa Babaker
"Kuna watu wanaounga mkono majadiliano, lakini wapo walioacha makazi yao wanaosema ni kwa msingi upi tunapaswa kujadiliana."
Babaker aliongeza kwamba "wanasema mtu aliniondoa nyumbani kwangu. Watu wengine wanasema wanaunga mkono majadiliano, kuna mitazamo tofauti."
Mapigano hayo yamemlaazimu mtu mmoja kati ya watano kuyahama makazi yao, huku mamia ya maelfu wakiuawa. Zaidi ya watu milioni 25 kote nchini humo wanakabiliwa na njaa kali, huku ukame ukitangazwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Darfur.