Jeshi la Ukraine laudhibiti mji wa Luhansk
21 Agosti 2014Msemaji wa serikali ya Ukraine, Andriy Lysenko, amesema jeshi la nchi hiyo limechukua udhibiti wa sehemu kubwa ya maeneo ya mji wa Luhansk unaodhibitiwa na waasi, ulioko umbali wa kilomita 20 kutoka kwenye mpaka wa Urusi.
Amesema pia ndege ya kivita ya Ukraine imedunguliwa leo kwenye mji wa Luhansk. Ndege hiyo ilikuwa ikuruka kwenye viunga vya mji huo, ingawa Lysenko amesema bado ni mapema mno kudhibitisha aliyehusika na shambulio hilo.
Tangazo la kudhibitiwa kwa mji wa Luhansk, limetolewa huku kukiwa na taarifa za kuwepo mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na waasi wanaoiunga mkono Urusi, karibu na Donetsk, ngome kuu ya waasi mashariki mwa Ukraine. Jana Jumatano, maafisa wa Ukraine walitangaza kuwa raia 43 wa eneo hilo waliuawa na wengine 42 walijeruhiwa wakati wa mapigano yaliyodumu kwa saa 24.
Wanajeshi tisa waliuawa kwenye mapigano hayo na wengine 22 walijeruhiwa katika mapigano ya usiku wa kuamkia leo kwenye eneo la Ilovaysk, karibu na Donetsk, ingawa vikosi vya serikali vimeendelea kusonga mbele na kuchukua udhibiti wote wa mji huo.
Poroshenko kukutana na Merkel
Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko anatarajiwa kukutana na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani mjini Kiev mwishoni mwa juma hili, kabla ya kukutana na Rais wa Urusi, Vladmir Putin wiki ijayo. Mkutano kati ya Poroshenko na Putin utakuwa ni wa kwanza kufanyika tangu mwezi Juni mwaka huu.
Jana, Rais Poroshenko alikutana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, anayeshughulikia masuala ya kisiasa, Jeffrey Feltman. Mkutano huo ulifanyika mjini Kiev, chini ya muongozo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi-UNHCR, limesema kiasi watu 415,800 wameyakimbia makaazi yao kutokana na mapigano hayo yanayoendelea mashariki mwa Ukraine. Kwa mujibu wa shirika hilo, zaidi ya watu 2,000 wameuawa tangu Aprili 6.
Ama kwa upande mwingine, Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu, limesema maafisa wa Ukraine wamechelewesha zoezi la kupeleka msaada wa kinaadamu wa Urusi mashariki mwa Ukraine, lakini juhudi za kuruhusu msafara wa malori yaliyobeba msaada huo kuendelea na safari, zinaendelea.
Msafara huo ulikwama kwenye mpaka wa Urusi na Ukraine kwa wiki sasa, baada ya ukraine kuwa na hofu huenda ukawa ni silaha zinazopelekwa kwa wapiganaji wanaoiunga mkono Urusi.
Wakati hayo yakijiri, Spika wa Bunge la Urusi, Sergei Naryshkin amesema leo kuwa mkutano kati ya viongozi wa Urusi, Ukraine na Umoja wa Ulaya utakaofanyika wiki ijayo mjini Minsk, ni hatua kubwa kuelekea kuumaliza mzozo wa Ukraine.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,APE,AFP,RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga