Joto kali na ukuaji wa miji, vinanatishia maisha ya mijini
5 Oktoba 2021Ripoti hiyo iliyochapishwa na jarida la Chuo cha Taifa cha Kisayansi Marekani inasema kuwa karibu robo ya idadi ya watu ulimwenguni wanaathirika na ongezeko la joto.
Katika miongo ya hivi karibuni, mamilioni ya watu wamehama kutoka maeneo ya vijijini na kuhamia mijini ambako joto kwa ujumla ni kali, kwa sababu ya kuwepo maeneo mengi yenye lami inayofyonza joto na ukosefu wa mimea.
Soma zaidWatu kadhaa wafa kutokana na joto kali Marekani na Canadai:
Wanasayansi walioandika ripoti hiyo walifanya uchunguzi wa viwango vya joto na unyevu wa kila siku katika miji zaidi ya 13,000 kutoka mwaka 1983 hadi 2016.
Kisha watafiti hao walilinganisha data za viwango vya hali ya hewa na takwimu za idadi ya watu mijini katika kipindi hicho cha miaka 33.
Cascade Tuholske kutoka Chuo Kikuu cha Columbia, ambaye pia ni mwandishi mkuu wa utafiti huo, amesema kupanda kwa joto pia kunaongeza magonjwa na vifo.
Joto linaporomosha uchumi
Aidha amesema joto kali linaathiri uwezo wa watu kufanya kazi, na kupelekea pato la kiuchumi la chini kuporomoka. Halikadhalika joto kali linachochea zaidi matatizo ya kiafya ambayo yalikuwepo tangu awali.
Ripoti hiyo imeshihirisha kwamba, ongezeko la idadi ya watu limechangia kwa theluthi mbili, na ongezeko la nyuzi joto limechangia kwa thuluthi moja kwa miji kuwa na joto kali.
Mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka, umetajwa kuwa ndiyo ulioathrika zaidi kwa kuwa na joto kali. Na hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu mjini humo, kutoka watu milioni nne mwaka 1983 hadi milioni 22 hii leo.
Miji mingine mikubwa imeonyesha hali hiyo hiyo, ikiwa ni pamoja na Shanghai, Guangzhou, Yangon, Dubai, Hanoi na Khartoum na pia miji kadhaa nchini Pakistan, India na Rasi ya Arabia.
Soma zaidi: China na Marekani zatoa ahadi mpya za kukabili joto duniani.
Aidha waandishi wa ripoti hiyo wanasema walichokigundua barani Afrika na Asia Kusini, kinaweza kupunguza faida za kiuchumi zinazopatikana mijini.
Kwa upande wa Marekani, miji mikubwa ipatayo 40 imeshuhudia joto kali hasa miji ya majimbo yaliyo kwenye Pwani ya Ghuba kama vile Texas, Louisiana, Mississippi, Alabama, na Florida.
Aidha wamesema kuwa kuna haja ya kuongeza uwekezaji mijini, na msaada wa serikali utahitajika ili kukabiliana na hali hiyo mbaya.