Jumuiya ya ASEAN yaadhimisha miaka 30 ya uhusiano wake
22 Novemba 2021Mkutano huo wa mtandaoni wa nchi wanachama wa Muungano wa Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia, au ASEAN, umefanyika kuadhimisha miaka 30 ya uhusiano kati ya China na kundi la nchi hizo wanachama wa ASEAN. China pia imesema itachangia dozi milioni 150 za chanjo ya Covid-19. Xi amesema nchi yake haitaendelea na siasa za kujikweza kimadaraka, licha ya luteka za jeshi la majini la nchi hiyo katika Bahari ya China Kusini eneo lililo na migogoro kadhaa ya kimaeneo inayoingiliana na majirani zake.
Rais Xi Jinping ameongeza kusema kuwa ni muhimu kuimarisha ushirikiano katika maeneo ya ulinzi, kukabiliana na ugaidi, utafiti wa pamoja wa baharini, uokoaji na mazoezi mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu wa kimataifa pamoja na kudhibiti majanga. Amesema juhudi za pamoja zinahitajika ili kulinda utulivu katika Bahari ya China Kusini na kulifanya kuwa ni eneo la amani, urafiki na ushirikiano.
Hivi majuzi, kulikuwa na malumbano mapya kati ya wanachama wa nchi za jumuiya ya ASEAN za Ufilipino, Malaysia na Vietnam katika maeneo ya bahari ndani na maeneo yanayoizunguuka bahari.
China inadai kuwa Eneo lote la Bahari ya China Kusini ni la kwake, imejenga visiwa bandia na kuvisheheni vifaa vya kijeshi. Nchi zinazozozana na China ni pamoja na Ufilipino, Vietnam, Malaysia, Brunei na Taiwan. Eneo hilo la bahari ya Kusini mwa China linaaminika kuwa na utajiri wa rasilimali za asili.
China imesema hatua yake ya kutangaza amani ni kwa ajili ya kuonyesha kuwa nchi hiyo inataka kuishi kwa amani na majirani zake na kufanya kazi pamoja ili kudumisha amani ya kudumu katika kanda ya Kusini-Mashariki mwa Asia.
Vyanzo:AP/DPA