Kiasi ya watu 150 wauawa katika ghasia za Haiti: UN
21 Novemba 2024Vifo hivyo vinafikisha idadi ya vifo nchini Haiti mwaka huu kupindukia 4,500. Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk ameonya katika taarifa kuwa ongezeko la karibuni la machafuko katika mji mkuu wa Haiti ni ishara ya hali mbaya zaidi ijayo.
Soma pia: Haiti: Polisi kwa kushirikiana na raia waua wanachama 28 wa genge la uhalifu
Amesema ghasia za magenge lazima zisitishwe mara moja. Machafuko yameongezeka katika mji wa Port-au-Prince tangu Novemba 11, huku mungano wa magenge ya wahalifu ukipambana kuchukua udhibiti kamili wa mji huo mkuu wa Haiti. Mpaka sasa magenge hayo yaliyojihami vikali yanadhibiti asilimia 80 ya mji huo.
Soma pia: WFP kuanza tena kupeleka msaada kwa ndege nchini Haiti
Yanawalenga mara kwa mara raia licha ya uwepo wa kikosi cha kimataifa cha polisi kinachoongozwa na Kenya. Taarifa ya Turk imesema pia kuwa kiasi ya watu 700,000 sasa wameachwa bila makao kote nchini humo, nusu yao wakiwa watoto.
Tayari, shirika la kimataifa la hisani la Madktari Wasio na Mipaka limesema limesitisha shughuli zake katika mji mkuu wa Haiti. Shirika hilo linaituhumu polisi ya Haiti kwa kuyasimamisha magari yao na kuwatolea wafanyakazi vitisho vya mauwaji na ubakaji.