Kifo cha Sinwar kinamaanisha ni kwa Hamas, Gaza, Lebanon?
20 Oktoba 2024Kwa maneno ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Yahya Sinwar, siku ya Jumatano yanamaanisha kuwa "Hamas haitatawala tena Gaza."
Kwa mtazamo wake, kifo cha Sinwar, ambacho kilithibitishwa Alhamisi, kinaashiria mwanzo wa "siku baada ya Hamas."
Hata hivyo, wachambuzi wanaona mustakabali tofauti kwa wanamgambo wa Hamas wanaoungwa mkono na Iran, ambao wameorodheshwa kama kundi la kigaidi na Marekani, Umoja wa Ulaya, na mataifa mengine mengi.
"Kifo cha Sinwar bila shaka ni pigo kwa Hamas kutokana na nafasi muhimu aliyokuwa nayo ndani ya kundi hilo," alisema Neil Quilliam, mshirika wa mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika kituo cha utafiti cha Chatham House kilichopo London, aliiambia DW.
Hata hivyo, Quilliam anasisitiza kuwa, hapo awali, sera ya kuondoa viongozi haijafanya lolote kudhoofisha nia na uwezo wa Hamas kupigana na Israel, kama ilivyotokea pale Sinwar mwenye umri wa miaka 61 aliposhika madaraka baada ya kuuawa kwa kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh, mjini Tehran mwezi Julai mwaka huu.
Soma pia: Hamas yamteua Yahya Sinwar kuchukuwa nafasi ya Haniyeh
"Hamas itajipanga tena kwa kuchagua kizazi kipya cha viongozi, kujijenga upya kijeshi na kiteknolojia, na kuwavutia vijana wa Palestina walioteswa na mgogoro na Israel huko Gaza na Ukingo wa Magharibi," alisema Quilliam.
Mtazamo huu unaungwa mkono na Peter Lintl, mtafiti katika Taasisi ya Ujerumani ya Mambo ya Kimataifa na Usalama (SWP). "Hamas bila shaka imelemazwa, lakini kifo cha Sinwar si pigo la mwisho kwa wanamgambo hao," aliambia DW.
'Fursa Iliyopotezwa'
Wakati huo huo, maafisa wa Ujerumani, Ufaransa, na Marekani wameonyesha matumaini kwamba kifo cha Sinwar kinaweza kuleta fursa ya kufanya makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.
Kuondolewa kwa Sinwar kwenye uwanja wa vita, "kunaweza kuleta fursa ya kupata njia ya kwenda mbele ambayo itawarejesha mateka nyumbani, kumaliza vita, na kutupeleka kwenye siku baada ya vita," alisema Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Jake Sullivan, Alhamisi.
Lakini Ijumaa, siku moja tu baada ya kuthibitisha kifo cha Sinwar, Hamas iliahidi kuendelea kuwashikilia mateka hadi vita vya Gaza vitakapomalizika.
Katika miezi 12 ya vita vya Gaza, vilivyochochewa na shambulio baya la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023, watu wapatao 42,000 wameuawa kulingana na mamlaka za afya zinazodhibitiwa na Hamas.
Na kati ya mateka wapatao 250 waliotekwa na wapiganaji wa Hamas mnamo Oktoba 7, takriban 100 wanadhaniwa bado wanaendelea kushikiliwa.
Hata hivyo, Mohammed al-Qawas wa kituo cha utafiti cha Emirates Policy Center (EPC) anachukulia kifo cha Sinwar kuwa mwanzo wa "sura mpya" ya vita vya Gaza.
"Mara tu majukumu ya mazungumzo ya usitishaji vita yanapohamishiwa kwa viongozi wa Hamas walio nje ya nchi, mazungumzo haya yatategemea mahesabu ya nje pia, kwa sababu viongozi hawa wote walio nje wanaathiriwa na miji mikuu wanamoishi, na labda ni kupitia miji hii mikuu Hamas inaweza kutoa muafaka na kuanzisha sera mpya," aliambia DW.
Uongozi wa kisiasa wa Hamas uko Qatar, lakini Sinwar mwenye msimamo mkali wa Gaza alikuwa ndiye mtu wao muhimu kwa mazungumzo ya usitishaji vita yaliyoongozwa na Marekani, Qatar, na Misri na Israel tangu kuuawa kwa Haniyeh.
Lintl wa SWP aliiambia DW kuwa licha ya kifo cha Sinwar, haoni sababu ya kutarajia kuwa Israel itakuwa tayari sasa kumaliza vita.
Soma pia:Blinken asema Sinwar anapaswa kusimamia makubaliano ya amani Gaza
Licha ya kusifia kifo cha Sinwar kama mwisho wa Hamas Alhamisi, Waziri Mkuu wa Israel, Netanyahu, pia aliweka wazi kuwa vita havitamalizika kabla ya viongozi wengine wa Hamas waliobaki – kama Mohammed Sinwar, kaka yake Yahya Sinwar na mrithi wake kama mkuu wa kijeshi wa Hamas – kuuawa na mateka wote waliobaki kurudishwa kutoka Gaza.
Kwa James M. Dorsey, mtaalam wa eneo hilo na mshirika mwandamizi katika Shule ya Mafunzo ya Kimataifa ya S. Rajaratnam na Taasisi ya Mashariki ya Kati huko Singapore, mtazamo huu ni "fursa iliyopotezwa."
"Badala ya kutumia mafanikio ya kijeshi ya Israel kutangaza ushindi Gaza, kushinikiza kusitisha mapigano ambayo pia yanaweza kumaliza uhasama Lebanon, na kujadili kubadilishana wafungwa ambako kungehakikisha kuachiliwa kwa mateka 101 waliobaki mikononi mwa Hamas, Waziri Mkuu Benyamin Netanyahu alisisitiza kuwa vita vitaendelea hadi jeshi la Israel litakapowakomboa mateka hao," aliandika katika chapisho lake la hivi karibuni kwenye blogu yake ya kisiasa, "The Turbulent World."
Zaidi ya Gaza — Kulipiza Kisasi kwa Hezbollah
Zaidi ya Gaza, Israel pia imeongeza mzozo wake na Hezbollah huko Lebanon baada ya mwaka wa mapigano madogo madogo.
Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran — ambalo Marekani na Ujerumani wameliorodhesha kama shirika la kigaidi, na tawi lake la kijeshi ambalo Umoja wa Ulaya unalitambua kama la kigaidi — linadai kuwa linaiunga mkono Hamas. Mnamo Septemba, Israel ilimuua kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah.
Wachambuzi wanaonyesha kuwa mauaji kama haya hayajasaidia kumaliza uhasama.
Soma pia: Kiongozi wa juu wa Hamas asema hawatarejesha mateka hadi Israel itakapomaliza vita
Baada ya kifo cha Sinwar kuwekwa hadharani Alhamisi, Hezbollah ilitangaza "awamu mpya na inayozidi kuongezeka" katika vita vyake na Israel, ikidai kuwa kwa mara ya kwanza imetumia makombora yanayoongozwa kwa usahihi kulenga Israel katika jaribio la "kuongeza mzozo siku baada ya siku."
Na siku ya Jumamosi, droni ya Hezbollah iliyashambulia makaazi binafsi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye alisema kundi hilo alilolitaja kuwa wakala wa Iran lilitaka kumuuwa pamoja na familia yake, na kuahidi kujibu vikali.